Habari

Ngumi na mateke hafla ya Ruto

March 7th, 2020 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAKABILIANO makali yalizuka katika hafla iliyoongozwa na Naibu Rais William Ruto katika Kaunti ya Murang’a wafuasi wa wabunge wa kundi la ‘Tangatanga’ walipokabiliana na wale wa Gavana Mwangi Wa Iria.

Dkt Ruto alikuwa amealikwa na mbunge wa Kandara, Alice Wahome kuongoza hafla ya kukabidhi Shule ya Upili ya Kinyoho basi.

Ghasia zilianza wakati Bw Wa Iria alivamia mkutano huo akiandamana na wafuasi wake baada ya kupata habari kwamba, wabunge wa Tangatanga waliokuwa wamehudhuria hafla nyingine katika eneobunge la Kandara walikashifu mswada wake kuhusu uzalishaji na uuzaji wa Avokado.

Wabunge hao walikuwa wamedai mswada huo unalenga kukandamiza wakulima.

“Tangu Bw Wa Iria alipoanza kuhudhuria mikutano feki ya BBI, ameanza kuwa na tabia za ajabu. Ni sharti aondoe mswada huo kwa sababu hauna cha kufaidi wakulima,” mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alisema akiwa kijijini Kiranga ambapo Dkt Ruto alifungua chuo cha kiufundi cha Kandara.

Wabunge waliohudhuria hafla hiyo walisema kuhusika kwa Wa Iria katika mchakato wa BBI unaoongozwa na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kulimchanganya hadi akatayarisha mswada huo.

Matamshi kama hayo yalitolewa na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira) na Bi Wahome wakisema gavana huyo anataka kutumia mlango wa nyuma kudhibiti sekta ya parachichi.

“Ikiwa Wa Iria anataka kuamua soko litakavyokuwa, aende katika shamba lake la parachichi, nitaleta magari yangu kununua avocado kesho,” Bw Kuria alisema.

Alipopashwa waliyosema, Bw Wa Iria alifika katika shule ya upili ya Kinyoho akiwa na wafuasi wake, lakini wakazuiwa kuingia ndani japo aliruhusiwa.

Walinzi wa Dkt Ruto na Mkuu wa upelelezi eneo la Muranga kusini (DCIO) walichukua hatua na kuanza kuwapiga wafuasi wa gavana huyo kwa mateke na mangumi.

Baadhi yao walipoteza fahamu baada ya ghasia zilizochukua dakika kumi.

Hali ya utulivu iliporejea, wabunge wanaomuunga Dkt Ruto walimlaumu Wa Iria kwa kuzua ghasia hizo wakisema alikuwa ametumwa na Bw Odinga kuvuruga mkutano huo.

“Hatuwezi kuruhusu wanasiasa waliotumwa na Bw Odinga kuvuruga mkutano wetu,” alisema mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Bw Wa Iria alipopatiwa nafasi ya kuzungumza, wafuasi wa Bi Wahome walianza kuimba nyimbo za kumkejeli huku wakimsifu Dkt Ruto.

Hata hivyo, gavana huyo hakuogopa na akahutubia umati.

“Nina haki ya kujibu madai dhidi yangu na hii ni kaunti yangu. Nimekuja kwa amani kujibu madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na baadhi ya viongozi kwamba ninalenga kukandamiza wakulima kupitia mswada wa parachichi. Ikiwa Bw Kuria na wenzake wanataka kununua parachichi kutoka Murang’a, basi anunue kwa zaidi ya Sh15, sitakubali yeyote kuchochea wetu,” alisema.