Nguo kuchanika K’Ogalo wakionana na Tusker FC

Nguo kuchanika K’Ogalo wakionana na Tusker FC

NA CECIL ODONGO

GOR MAHIA na Tusker leo Jumatano zitavaana kwenye mechi kali ya Ligi Kuu (KPL) itakayosakatwa katika uga wa Kasarani kuanzia saa tisa mchana.

Ligi hiyo inaingia raundi ya 15 leo na kesho huku mechi saba zikisakatwa leo Jumatano na nyingine mbili Alhamisi.

Viongozi wa ligi, Nzoia Sugar watakuwa ugenini dhidi ya Kariobangi Sharks ugani Utalii.

Ni mechi moja pekee ambayo ni kati ya Bandari na Kakamega Homeboyz itakayosakatwa nje ya Nairobi. Timu hizo zitachuana ugani Mbaraki, Kaunti ya Mombasa.

Mabingwa mara 12, AFC Leopards nao watakuwa ugenini dhidi ya FC Talanta katika uga wa MISC Kasarani. Mathare United na Vihiga Bullets ambazo zinakokota nanga mkiani mwa FKF-PL nazo zitachuana katika uga wa Ruaraka.

Mbio za kusaka kiatu cha dhahabu nazo zinatarajiwa kushika kasi kwa mara nyingine kati ya Benson Omala wa Gor Mahia na Elvis Rupia wa Kenya Police.

Omala amecheka na nyavu mara 11 huku Rupia ambayo timu yake inavaana na Nairobi City Stars ikiwa imeyafunga mabao 10.

Mechi kati ya Tusker na Gor huwa si rahisi ikizingatiwa kuwa huwa imejaa uhasama mkubwa na ushindani mkali.

K’Ogalo inashikilia nafasi ya pili kwa alama 27, pointi moja nyuma ya Nzoia Sugar ila ina mechi mbili kiporo.

KCB ambayo ni ya pili kwa alama 27 ila inadunishwa na mabao na imecheza mechi 14. Iwapo KCB itapata ushindi kisha Nzoia na Gor zidondoshe alama, basi itapaa kileleni mwa jedwali la KPL.

Tusker ilianza msimu kwa kishindo huku ikishinda mechi zote tisa za mwanzo. Hata hivyo, timu hiyo imeingiwa na kutu huku ikishinda mechi moja pekee kati ya saba zilizopita.

Tusker inashikilia nafasi ya tano kwa alama 25 na wanalenga kurejelea makali yao ikizingatiwa ushindi wao wa mwisho ulikuwa dhidi ya Sofapaka mnamo Januari 22.

Gor nayo inaelekea katika mechi dhidi ya Tusker ikisaka ushindi kwa kuwa haijawahi kufanya hivyo dhidi ya wapinzani hao katika mechi tano zilizopita. K’Ogalo iliishinda Tusker mara ya mwisho mnamo Agosti 31, 2019.

Katika mechi hizo tano Tusker imeshinda mara tatu huku mbili zikiishia sare.

Msimu jana, mashabiki wa Gor Mahia walizua vurugu katika uwanja wa Kaunti ndogo ya Thika katika mechi yao dhidi ya Tusker na kurusha mawe. Tusker pia walimkaba koo refa wa katikati ya uwanja katika mchuano huo baada ya kukubali kisha tena kukataa bao la Jackson Macharia sekunde ya mwisho ya mtanange huo.

“Tunajua kuwa Tusker haijakuwa na misururu ya matokeo mazuri. Sisi tumepoteza mara moja pekee msimu huu na ni vyema tuendelee kusajili matokeo hayo mazuri,” akasema Kocha wa Gor Johnathan McKinstry.

Naye nahodha wa Tusker Humprey Mieno alisema,”Tunapokabili Gor, tunastahili kuwa sawa kisaikolijia na kusahau matokeo duni ambayo yamekuwa yakituandama. Nina hakika kila moja wetu atajituma ili tupate ushindi.”

Iwapo Gor itashinda kisha Nzoia Sugar idondoshe alama basi itapaa kileleni mwa KPL.

Nzoia nayo ina rekodi nzuri dhidi ya Sharks ikiwa imeshinda mechi zote tatu zilizokutanisha timu hizo mtawalia. Sharks wikendi iliyopita waliandikisha sare ya 1-1 dhidi ya Tusker katika uga wa Ruaraka.

Leopards nayo itafikisha alama 25 iwapo itaichapa FC Talanta hapo kesho Alhamisi.

Ingwe ilazimisha sare dhidi ya viongozi Nzoia Sugar katika uga wa Sudi mnamo Jumapili.

Kwa sasa Ingwe ni nambari saba kwa alama 22 baada ya mechi 14. FC Talanta nao wapo nambari 14 kutokana na alama 12 baada ya mechi 13.

Msimu uliopita, Leopards ilishinda mkondo wa pili 3-2 baada ya mkondo wa kwanza kuishia sare ya 1-1.
Mathare United na Vihiga Bullets nazo zina alama nne kila moja baada ya kuwajibikia mechi 11.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Hasla Fund yanyofolewa Sh40 bilioni kinyume na...

Hali ya Man City si shwari tena

T L