Makala

NGURE: Kuundwa Baraza la Kiswahili itakuwa tuzo kwa Walibora

April 16th, 2020 3 min read

NA ALEX NGURE

TUNAFURAHI sana tukiangalia vile Kiswahili kilivyopiga hatua lakini watu wajue kuwa ukiona vinaelea ujue vimeundwa.

Kiswahili kimetoka mbali na kimefanya watu wengi watoe jasho katika kukikuza. Kiswahili kimekuwa na vikwazo vya hapa na pale lakini wapenzi wake kama Ken Walibora walifunga vibwebwe kweli kweli hadi kukifikisha kilipo leo hii.

Ukweli ni kwamba Kiswahili kimepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, safari bado ni ndefu. Imedhihirika kwamba katika kila kongamano linaloandaliwa nchini Kenya, mapendekezo mengi muhimu yameafikiwa na wataalamu wanaohudhuria kuhusu mustakabali wa Kiswahili.

Mojawapo ya mapendekezo hayo ni dharura ya kuundwa kwa chombo cha Kiserikali kinachoweza kutwikwa jukumu la kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini Kenya. Wanaohudhuria makongamano haya hutoka huko kwa matumaini makubwa kwamba punde si punde, utafuata mchakato mzima wa kuhakikisha yanayopendekezwa yanatekelezwa.

Ken Walibora alikuwa mojawapo wa wataalamu ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Bunge linaunda sera ya lugha na Baraza la Kiswahili nchini Kenya (BAKIKE)- mithili ya Baraza la Kiswahili la Taifa-Tanzania (BAKITA), ambalo litakuwa mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili.

Hatua ya Kenya kukiteua Kiswahili kuwa lugha ya taifa na pia lugha rasmi sambamba na Kiingereza haitoshi iwapo haitaungwa mkono kikamilifu na mfumo wa siasa na nadharia-endelezi za Kiswahili nchini Kenya.

Imepita miaka kumi tangu Katiba mpya iliporasimishwa. Tulitarajia kwamba hali hiyo ingeharakisha kuundwa kwa vyombo vya utekelezaji, lakini hakuna hatua yoyote ya haja iliyokwisha pigwa kufikia sasa. Kama kuna suala linalohitaji kushughulikiwa kwa dharura na Wabunge ni uundaji wa vyombo vya Kiserikali vitakavyofadhiliwa na serikali, ambavyo vitakipa Kiswahili na watumizi wake mwongozo mwafaka.

Katika makala yake ya mwisho katika Taifa Leo, Ken Walibora anasema: ‘Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili njia pekee ya kuenzi wafia lugha’ (Taifa Leo tarehe 15.4.2020). Kama kuna mfia lugha atakayekumbukwa daima ni Ken Walibora. Kwa hivyo, kuundwa kwa Baraza la Kiswahili ndiyo itakuwa njia bora ya kumuenzi mwendazake Ken Walibora manake hii ndiyo iliyokuwa kauli yake ya mwisho.

Katika makala haya, Ken anamtaja Mtumishi Njeru Kathangu kama mbunge aliyezungumza Kiswahili bungeni japo hakuwa mzawa wa Uswahilini. Hata katika bunge la sasa kuna wabunge kama vile Mohammed Ali almaafu Jicho Pevu na wengineo, walio na ghera na ari ya kuzungumza Kiswahili bungeni.

Wabunge

Hata hivyo, ajabu ni kwamba baadhi ya Wabunge wanaotoka katika maeneo ambayo ndiyo chimbuko na kitovu cha Kiswahili, wanakionea haya Kiswahili. Hawatoi hoja zao kwa Kiswahili bungeni. Nchini Tanzania mijadala yote bungeni; ukiwemo usomaji wa bajeti na shughuli zote rasmi za serikali hufanywa kwa Kiswahili.

Katika vyombo vya habari, wasikilizaji na watazamaji wanaoongea Kiswahili wanahiniwa wakati ambapo mijadala mingi ya kitaaluma ama yenye umuhimu wa kitaifa kama vile janga la corona, inapoendeshwa kwa Kiingereza. Aghalabu wanapouliza maswali kwa Kiswahili, wanapuuzwa ama wanajibiwa kwa Kiingereza. Si ajabu basi kwamba, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiruhusu Kiswahili kutumiwa kama lugha ya mizaha isiyozingatia kanuni za sarufi na lugha kwa ujumla.

Jambo la kuvunja moyo ni kwamba hadi kufikia sasa, kuna vita baridi miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili kuhusu nani anafaa kushughulikia ukuzaji wa lugha. Jambo hili linarudisha maendeleo ya lugha hii nyuma. Wachache wanaojinasibisha na lugha hii wanajiona ni bora kuliko wanagenzi wa lugha na hawashirikiani nao katika kukuza lugha.

Wazee wakwasi wa lugha kama marehemu Shiekh Nabahany na Hassan Mwalimu Mbega walipuuzwa mara kwa mara na hawakupewa nafasi katika kuendeleza lugha.

Ken Walibora daima alisikitika kwamba muungano kamili wa wasomi wanaofaa kuwa mstari wa mbele katika uendelezaji wa Kiswahili bado haujapatikana. Prof Walibora alihimiza:

‘Badala ya kushirikiana na kusaidiana kukuza hii lugha yetu inayozungumzwa na mamilioni ya watu na kufunzwa katika vyuo vingi kote duniani; kuna dharau na ndaro za ajabu pamoja na mashindano mengi yasiyosaidia maendeleo yake.

Badala ya kuongozana; wivu, ubinafsi, fitina na uongo vimetawala baadhi ya watu. Ukisema neno fulani ni Kiswahili unaambiwa unaongea kikwenu! Taabu zote hizi zitakapopungua au kwisha kabisa, ndipo Kiswahili kitakapozidi kukua na kupendwa. Jamani tunajenga nyumba moja, tusipiganie fito’ anamalizia mwendazake Walibora.

*Natumia fursa hii kutoa rambirambi zangu za dhati kwa familia, jamaa, marafiki na jamii nzima ya Kiswahili kwa kupotelewa na Ken. MAKIWA!