Kimataifa

Nguruwe wamla mama aliyewalisha

February 8th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE wa miaka 56 kutoka Urusi aliliwa hadi kufa na nguruwe wake waliokuwa njaa katika zizi walimoishi, wakati alienda kuwalisha chakula.

Mkulima huyo ambaye hakutajwa anaripotiwa kutoka eneo la Udmurtia na aliliwa hadi akazirai, kisha baadaye akakata roho, polisi wamesema.

Kulingana na ripoti za polisi, mwanamke huyo alivamiwa na nguruwe hao waliokuwa na njaa na wakatafuna uso wake kabisa, masikio na mabega.

Alifariki baadaye kutokana kupoteza damu nyingi mwilini katika hospitali ya wilaya ya Udmurtia, Malopurginsky.

Mumewe alikuwa mgonjwa na alipoamka alishangaa kumkosa marehemu. Hata hivyo, alipoenda kumtafuta baadaye, alipata mwili wake ukiwa umeliwa katika zizi la nguruwe hao.

Wachunguzi katika kesi hiyo walisema hawajawahi kushuhudia kisa cha aina hiyo, haswa katika miaka ya majuzi na kuwa kiliwashangaza watu wengi.

Kisa hicho kiliacha familia na eneo husika katika majonzi na mshtuko, wengi wasiamini kuwa ulikuwa ukweli.