NGUVU ZA HOJA: Jinsi Kiswahili kilivyotumiwa na wanasiasa kueleza sera zao

NGUVU ZA HOJA: Jinsi Kiswahili kilivyotumiwa na wanasiasa kueleza sera zao

PROF JOHN KOBIA

WAKENYA waliwachagua viongozi wao wa kisiasa tarehe 9 Agosti mwaka huu.

Viongozi wa kisiasa walitumia lugha mbalimbali kuwarai wapiga kura kuwaunga mkono. Katika ngazi ya kitaifa, lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya kuwaunganisha Wakenya katika mchakato wa kupiga kura.

Lugha ya Kiswahili ina mchango mkubwa katika kufanikisha sera, ajenda na manifesto ya kisiasa nchini Kenya. Ingawa manifesto ya vyama vya kisiasa ziliandikwa kwa Kiingereza, walitumia Kiswahili katika kusisitiza masuala yenye umuhimu ili kuwashawishi wapiga kura. Kwa mfano, majina ya vyama miungano ya vyama ina majina kwa Kiswahili. Kwa mfano, Azimio la Umoja, Kenya Kwanza, Agano.

Majina haya husisitiza mwongozo wa vyama hivi.

Vilevile kaulimbiu za vyama vya kisiasa zilifafanuliwa kwa kutumia Kiswahili. Kwa mfano, Inawezekana, Kazi ni kazi na kadhalika.

Kauli mbiu hizi zilitumiwa kuwaleta wananchi pamoja, kusisitiza umoja na kuhimiza matumaini ya siku zijazo.

Wanasiasa walitumia Kiswahili kama lugha yenye mvuto ili kuwahamasisha wapiga kura kuhusu sera zao za kisiasa.

Nyimbo za kisiasa zilitungwa kwa Kiswahili na kuwasilishwa kwa wananchi ili kuwavutia katika mikutano ya kiasa.

Waimbaji wengi walivuna mapato kutokana na uwasilishaji wa nyimbo wakati wa kampeni za kisiasa. Nyimbo hizi ziwasisimua sana wafuasi wa mirengo tofauti.

Wanasiasa walitumia lugha ya Kiswahili kujijenga kisera na vilevile kuwabomoa wapinzani wao kisiasa. Kiswahili ni lugha inayoweza kutumiwa na wanasiasa ili kuhakikisha wanaendelea kubaki kwenye mamlaka.

Isitoshe, wanasiasa walibuni na kutumia maneno Kiswahili kuwasuta na kuwakejeli wapinzani wao.

Pia, walibuni maneno ya kuwazindua na kuwarai wafuasi wao kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

Wanasiasa walitumia Kiswahili ili kuwafahamisha wananchi kuhusu masuala muhimu katika manifesto zao. Baadhi ya masuala ni ufisadi, usalama, haki za binadamu, uchumi (pesa mfukoni), afya, umaskini na mengineyo.

Huenda namna masuala haya yalivyowasilishwa kwa Kiswahili kulichangia matokeo ya upigaji kura yanayobainika.

Lugha ya Kiswahili ina mchango kwa wanasiasa ili kupata uwezo na mamlaka ya uongozi wa kisiasa nchini Kenya.

John Kobia ni mtunzi wa Kamusi Bora ya Watoto

  • Tags

You can share this post!

Uchaguzi 2022: Ruto, Raila wafuatana kwa karibu kura...

KINYUA BIN KING’ORI: Tumefanya uamuzi wetu kwenye...

T L