NGUVU ZA HOJA: Kinaya cha Kiswahili kuenziwa mno ughaibuni kuliko nyumbani!

NGUVU ZA HOJA: Kinaya cha Kiswahili kuenziwa mno ughaibuni kuliko nyumbani!

NA PROF IRIBE MWANGI

KATIKA diwani yake Kina cha Maisha, Said Ahmed ameandika shairi “Hatuzwi Mcheza Kwao.” Anwani hii ni kinyume cha methali “Mcheza kwao hutuzwa.”

Ni katika diwani hii pia ambapo kuna shairi “Kinyume Mbele.” Awali sikuelewa sababu ya mwandishi kuchukua mkondo huu wa fikira. Kwa sasa naelewa fika!

Katika safari yangu Marekani, nimetambua kwamba lugha ya Kiswahili inaenziwa sana! Wengi wanajifunza na kufurahia Kiswahili, wengine hata wanalipa ili kujifunza. Kevin Machine wa Swahili Cultural Village jijini New York analielewa hili vizuri.

Jumapili iliyopita niliungana na kundi la Wakenya jijini St Louis, Missouri, kwa hisani ya Prof Mungai Mutonya na Geoffrey Soyiantet wa Vitendo 4 Africa. Walikuwa na hamu kubwa kujua kuhusu Kiswahili: mambo yalikuwa vipi siku za nyuma? Kwa sasa tuko wapi kukihusu? Kuna mipango ipi ya baadaye kuhusu maendeleo ya Kiswahili nchini Kenya, katika kanda ya Afrika Mashariki, barani Afrika na duniani kote?

Wapenzi hawa wa Kiswahili walinieleza kuhusu faida inayoweza kutokana na maenezi ya Kiswahili ulimwenguni.

Walisisitiza haja ya Kenya kuongoza katika mustakabali wa kupigia debe Kiswahili. Hata hivyo, walifurahi kwamba sifa kinazopata Kiswahili, kwa mfano kuteuliwa kwa Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, zinafanya bara la Afrika kuangaziwa zaidi. Nilifurahi kuona kuwa kuna vyombo vya habari vinavyolenga Wakenya, kama vile KDM, vilivyotenga muda kutumia Kiswahili. Kwa hili nawashukuru Jeremmy Damaris, Michael Taasiri pamoja na Wilfred Kimani.

Nimetambua kwamba japo Kiswahili hakituzwi kwao, ugenini kinaenziwa sana!

You can share this post!

Wakili anayedaiwa kusema polisi ni mbwa ashtakiwa kwa...

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Heko Mama Samia, Dkt Ruto na...

T L