NGUVU ZA HOJA: Tujifunze Kiswahili kutoka kwa wazee mikota wenye tajiriba pevu

NGUVU ZA HOJA: Tujifunze Kiswahili kutoka kwa wazee mikota wenye tajiriba pevu

NA PROF IRIBE MWANGI

JUMATATU nilikuwa na kikao na watu muhimu katika ulimwengu wa Kiswahili.

Mmoja wao ni Balozi Wanjohi, Mkurugenzi wa Diplomasia ya Utamaduni katika Wizara ya Maswala ya Kigeni na Dayaspora.

Balozi Wanjohi amekuwa mpenzi na shabiki mkubwa wa Kiswahili na kuna matumaini kwamba atasaidia katika usambazaji wa Kiswahili hasa kupitia balozi zetu. Wa pili alikuwa mwanahabari na gwiji wa Kiswahili Nuhu Bakari. Anasifika zaidi kwa utunzi na ulumbi wa ushairi. Binafsi humwita tu Bingwa!

Wa tatu ni jagina, ustadh, gogo, gwiji na Profesa wa Kiswahili. Ni mwandishi, mwalimu na mshairi shupavu. Mara ya mwanzo “nilipokutana” naye, nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Ilikuwa kwa hisani ya Profesa Kineene wa Mutiso aliponitanguliza kwa dafina iitwayo Sauti ya Dhiki. Namzungumzia Mzee Abdilatif Abdala. Alikuwa kati ya wafungwa wa kwanza kabisa wa kisiasa nchini mnamo 1968 alipoandika makala “Kenya twenda wapi?” Nilipoyasoma mashairi yake, nilipata taswira ya mtu mkali, mwenye vurugu na fujo. Taswira hii iliyeyuka nilipokutana naye mara ya kwanza nchini Ujerumani mnamo 2016. Nilishtukia kuwa ni mtu mpole, mcheshi na maridhia.

Jambo muhimu nililolisoma kutokana na kikao chetu ni kina cha mawazo alichonacho Abdilatif. Katika kikao hicho, tulijifunza mengi kuhusu Kiswahili kutoka kwake. Ni hazina muhimu na naomba kwamba tunapokuwa na mikutano na hafla za Kiswahili tusiwasahau wazee kama hawa ili Kiswahili kinufaike kutoka kwao. Wenyewe ni dafina kuu lakini ni wanyenyekevu na hivyo hawajipigii debe!

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Nelson Mandela

NGUVU ZA HOJA: Hadhari iwepo katika kubuni maneno ya lugha...

T L