NGUVU ZA HOJA: Umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani

NGUVU ZA HOJA: Umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani

NA PROF CLARA MOMANYI

TANGAZO la UNESCO kwamba tarehe 7 Julai itakuwa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani bila shaka liliwasisimua si tu wenyeji wa Afrika Mashariki bali pia barani Afrika.

Tangazo hili lilitolewa mnamo tarehe 23 Novemba mwaka jana katika Kikao cha 41 cha nchi wanachama jijini Paris, Ufaransa. Mitandao ya kijamii ilisaki kauli na hoja mbalimbali kushabikia hatua hiyo adhimu iliyochukuliwa na Shirika ambalo kwa hakika huzingatia sana makuzi na uhifadhi wa lugha asilia za ulimwengu.

Shirika hili pia ni miongoni mwa Mashirika ya Kimataifa yanayohimiza umoja ndani ya uanuwai wa lugha za ulimwengu, ukiwemo uhuru wa mtu kujieleza kwa lugha yoyote anayoiteua. Katika muktadha huu pia, kurasa za historia ya ulimwengu zinaonyesha bayana kwamba hakuna lugha yoyote ya Kiafrika iliyoteuliwa hapo awali ili kusherehekewa na Umoja wa Mataifa.

Kwa hivyo, hii ni taadhima na heshima kubwa tuliyotunukiwa sisi kama wenyeji wa Afrika Mashariki ambako Kiswahili kiliasisiwa. Umuhimu wa maadhimisho haya si tu kutambua msambao wa Kiswahili ulimwenguni bali pia kutambua nafasi ya Kiswahili katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya mawasiliano hususan ya kiteknolojia na kidijitali.

Ni wazi kwamba Kiswahili kinafundishwa katika taasisi nyingi ulimwenguni, vikiwemo vyuo vikuu. Kwa mfano, nchini Marekani, takriban vyuo na taasisi mia mbili hufunza Kiswahili kama somo na wanafunzi wengi hushabikia masomo ya Kiswahili.

Soko la mauzo ya Kiswahili kama bidhaa au kitega uchumi litapanuka kwani watu wengi wakiwemo wageni kutoka ughaibuni na wale walio ughaibuni watashabikia Kiswahili kiasi cha kutaka kufunzwa lugha hii. Nchi za Afrika Mashariki bila shaka zitafaidika iwapo zitaweka mikakati ya kukiuza Kiswahili kama bidhaa. Tufahamu pia kwamba ajizi ni ufunguo wa umaskini.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Ikiwa Sheng ni kizawa cha Kiswahili,...

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukitumia ubongo wako vizuri...

T L