Nguvu za Ruto Mlimani zatikisa usemi wa Rais

Nguvu za Ruto Mlimani zatikisa usemi wa Rais

USHINDI mkubwa wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya kwenye uchaguzi uliofanyika Jumanne, umemweka Rais Uhuru Kenyatta na mabwanyenye kutoka eneo hilo katika njia-panda ya kisiasa.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufikia sasa, chama cha UDA, cha Dkt Ruto, kimepata ushindi mkubwa katika kaunti zote 10 za ukanda huo, ikilinganishwa na chama cha Jubilee, anachoongoza Rais Kenyatta.

Kaunti za Mlima Kenya zinajumuisha Nyeri, Nyandarua, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Embu, Meru, Tharaka-Nithi, Laikipia na Nakuru.

Kwenye uchaguzi huo, wanasiasa wengi ambao walikuwa washirika wa Rais Kenyatta walipoteza nyadhifa zao, baada ya ‘kusombwa’ na wimbi la UDA.

Katika Kaunti ya Nyandarua, Gavana Francis Kimemia (Jubilee) alishindwa na Kiarie Badilisha (UDA); Nyeri, Gavana Mutahi Kahiga (UDA) alihifadhi nafasi yake; Kiambu, Gavana James Nyoro (Jubilee) alishindwa na Kimani Wamatangi (UDA); Murang’a, Irungu Kang’ata (UDA) aliibuka mshindi; Kirinyaga, Bi Anne Waiguru (UDA) alimshinda Bi Wangui Ngirichi (mwaniaji huru) ijapokuwa aliyeonekana kuegemea mrengo wa Azimio huku Embu, Bi Cecily Mbarire (UDA) akaibuka mshindi.

Katika Kaunti ya Meru, Bi Kawira Mwangaza (mwaniaji huru) alimshinda Gavana Kiraitu Murungi (Azimio); Tharaka Nithi, Gavana Muthomi Njuki (UDA) akahifadhi kiti chake; Laikipia, Bw Joshua Irungu (UDA) akamshinda Gavana Nderitu Muriithi (PNU, Azimio) huku Bi Susan Kihika (UDA) akimshinda Gavana Lee Kinyanjui (Jubilee).

Mbali na ugavana, UDA ilishinda idadi kubwa ya maseneta, wawakilishi wa kike, wabunge na madiwani.

Katika taswira hiyo, wadadisi wa siasa wanataja mwelekeo huo mpya kuwa mtihani mgumu wa kisiasa kwa Rais Kenyatta, washirika wake wa kisiasa na mabwanyenye waliomuunga mkono, kwani huenda akakosa usemi wa kisiasa aliokuwa nao hapo awali.

Hili ni ikizingatiwa kuwa kwenye mahojiano na vituo vya redio na televisheni vinavyotangaza kwa lugha asili za eneo hilo wiki iliyopita, Rais alisema kuwa “hataenda mahali.”

“Siendi mahali. Ni anwani tu nimebadilisha. Nitakuwa tayari kushiriki kwenye juhudi za kuwasaidia watu wetu wakati wote nitakapohitajika,” akasema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, wadadisi wanaeleza Rais Kenyatta atakuwa na kibarua kigumu kutimiza hilo, kwani tayari wenyeji wameonekana “kumuasi kisiasa”.

“Katika hali ambapo UDA inaonekana kudhibiti siasa za ukanda huo, itakuwa vigumu sana kwa Rais kuendeleza ushawishi wake wa kisiasa. Taswira iliyopo ni kama ya mwanamume aliyetorokwa na mke na watoto wake,” asema Bw Oscar Plato, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana na matokeo hayo, Jubilee imefanikiwa kupata chini ya viti kumi vya ubunge.

Kinaya ni kuwa, baadhi ya watu walioonekana kujitokeza pakubwa kumtetea Rais Kenyatta na kuendeleza kampeni zake walishindwa kutetea viti vyao.

Baadhi yao ni wabunge Jeremiah Kioni (Ndaragwa), Kanini Keega (Kieni), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) kati ya wengine.

“Mwelekeo huu unaonyesha kuwa Rais Kenyatta amepoteza usemi na ushawishi wake wa kisiasa aliokuwa nao hapo awali kama vile katika chaguzi za mwaka 2013 na 2017. Itamlazimu kuanza mkakati mpya kurejesha nafasi yake,” akasema Bw Plato.

Hata hivyo, baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta wanasema kuwa hakuna lolote ambalo wamepoteza, bali ushindi wa Dkt Ruto unatokana na “uwongo aliowapa wenyeji wa Mlima Kenya”.

“Ukweli ni kuwa Rais Kenyatta hakushindwa. Wenyeji wataanza kubadilisha misimamo yao baada ya kubaini uwongo walioambiwa dhidi ya viongozi wao. Bado kuna nafasi kubwa Rais Kenyatta kurejesha usemi wake baada ya uhalisia kamili kufahamika,” asema Bw Keega.

  • Tags

You can share this post!

Barasa kortini kudai fidia baada ya IEBC kuahirisha uchaguzi

Chebukati ataka polisi wachunguze aliko afisa

T L