Habari za Kitaifa

NHIF: Hitilafu yachelewesha, kukosesha wagonjwa huduma

March 27th, 2024 1 min read

CHARLES WASONGA Na LINET OWOKO

WAGONJWA wanaotumia kadi za Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) kupata huduma za matibabu au kuzilipia Jumanne walikumbwa na shida kufuatia hitilafu katika mitambo ya asasi hiyo.

Hali hiyo ilidumu kwa saa kadhaa.

Maelfu ya wagonjwa, waliotarajia kulipia bili zao kutumia kadi ya NHIF, walilazimika kulipa pesa taslimu au kusubiri hadi huduma kupitia mitambo hiyo iliporejeshwa.

Duru katika NHIF zilifichua kuwa hitalifu hiyo iliripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo Jumatatu jioni na haikuwa imetatuliwa kufikia Jumanne jioni.

NHIF ilithibitisha hitilafu hiyo huku maelfu ya wagonjwa wakitumia mitandao ya kijamii kuwasilisha malalamisho yao.

Baadhi yao walisema walikosa huduma muhimu ya kimatibabu baada ya malipo yao kufeli kutayarishwa na hivyo kusababishia machungu zaidi.

“Hujambo, kutokana na hitilafu ya kiufundi, huduma itakawia. Tunaomba msamaha kwa usumbufu uliosababishwa na hali hii,” NHIF ikasema katika ujumbe mfupi kwa watu waliosajiliwa kwa bima hiyo ya matibabu.

“Tutawajulisha baada ya muda mfupi kuhusu ni lini huduma zitarejea kama kawaida,” ikasema sehemu ya ujumbe mwingine uliotumiwa wanachama wa NHIF.

Hitilafu hii inajiri wakati ambapo asasi inadaiwa hadi Sh6 bilioni na hospitali kadhaa nchini, hali ambayo imezilazimisha kulazimisha wagonjwa wenye kadi za NHIF kulipa pesa taslimu ili wapate huduma mbalimbali.