Habari Mseto

NHIF kugharimia matibabu ya wagonjwa wa Covid-19 hospitali za serikali

July 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NI afueni kwa wagonjwa wa Covid-19 baada ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF) kusema itagharimia matibabu yao katika hospitali za serikali.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa hazina hiyo Peter Kamunyo amesema bili za matibabu za watoto wa wagonjwa hao pia zitalipwa endapo watatibiwa katika hospitali za serikali zinazotambuliwa na Wizara ya Afya.

Hospitali hizi ni pamoja na: Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Hospitali ya Mbagathi. Hizi zinahudumia wagonjwa wa Covid-19.

Zingine ni hospitali za kaunti na vituo vingine vya afya vinavyotambuliwa na Wizara ya Afya.

“NHIF haitalipa gharama ya matibabu katika vituo vya afya ambavyo havitambuliwi na Wizara ya Afya,” Bw Kamunyo akasema.

Mnamo Machi 2020 kampuni za bima nchini zilikubali kugharamia bili za matibabu ya Covid-19 lakini baadaye zikabadili msimamo.

Katika siku za hivi karibuni kampuni hizo zimekuwa zikiagiza hospitali mbalimbali kutokubali kadi za zikisema kanuni haziwaruhusu kulipia gharama ya magonjwa ambayo yametangazwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama janga.

Lakini Jumanne NHIF ilisema hivi: “Afya ni wanachama wetu ni muhimu zaidi kwetu. Kwa hivyo, kama njia ya kupiga jeki juhudi za serikali za kudhibiti Covid-19, tutagharamia matibabu ya wagonjwa wa corona watakaolazwa katika hospitali zinazotambliwa na Wizara ya Afya.