Habari za Kitaifa

NHIF yamulikwa kwa dili feki za Sh21 bilioni kutibu wagonjwa

January 7th, 2024 2 min read

DAVID MWERE NA CHARLES WASONGA

BIMA ya Kitaifa ya Afya (NHIF) inamulikwa baada ya zaidi ya Sh21 bilioni kutolewa kutoka hazina yake kulipa madai feki ya huduma za afya zilizotolewa na hospitali mbalimbali.

Madai hayo yako kwenye malalamishi yaliyowasilishwa bungeni na mshauri kuhusu Udhibiti wa Ulaghai katika asasi za umma Bw Bernard Muchere.

Anawataka wabunge wachunguze visa vya ufyonzaji pesa za umma katika NHIF kupitia ulipaji wa madai ghushi yaliyowasilishwa na hospitali husika.

Bw Muchere anadai kuwa alipofanya uchunguzi wa ubadhirifu kwenye taarifa za fedha za NHIF, alibaini kuwa wakati wa kuandaa taarifa za fedha za mwaka wa fedha 2021/22, rekodi ilionyesha kuwa zaidi ya Sh21 bilioni zilitumika bila kuratibiwa.

Kulingana na Bw Muchere, rekodi hiyo ya NHIF iliundwa kwa usaidizi wa kampuni ya huduma za fedha, Kenbright Actuarial and Financial Services na miaka kubadilishwa na kuwekwa ya 2019/2020 pamoja na miaka ya kifedha iliyotangulia.

Walalamishi wanasema madai haramu yanayowasilishwa kwa NHIF na baadhi ya hospitali yamesababisha changamoto za kifedha katika asasi hiyo kiasi kwamba imeshindwa kulipa bili za matibatu kwa wachangiaji halali katika bima hiyo.

Hali hiyo imechangia visa vya idadi kubwa ya wagonjwa kunyimwa matibabu katika baadhi ya hospitali zilizosajiliwa na NHIF.

“Uovu kama huu ulichangia NHIF kulipa mamilioni ya fedha kwa wagonjwa feki badala ya wagonjwa halisi,” anasema Bw Muchere.

Alipendekeza kuwa wahusika katika wizi wa pesa hizo za umma wachunguzwe na wabunge na ikiwezekana waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

Mwaka jana, 2023, NHIF ilibadilishwa jina kuwa Mamlaka ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIA) baada ya sheria kufanyiwa mabadiliko.

Walalamishi wanasema kuwa ukweli unaonyesha kuwa “NHIF imezongwa na hatari ya ulaghai na wizi wa pesa.”

Wanaelezea hofu kwamba hata ingawa Sheria ya NHIF imefanyiwa mabadiliko kuna uwezekano mkubwa kuwa mamlaka ya SHIA isiposimamiwa vizuri itakumbwa na njama ya wizi wa pesa yanayozonga NHIF na “wagonjwa wataendelea kuteseka.”

Bw Muchere pia anawataka wabunge kubaini ikiwa Waziri wa Afya, aliyekuwa wakati pesa hizo zilifyonzwa, alitoa idhini zilipwe.

Mnamo Desemba 8, 2023 Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula aliiagiza Kamati ya Bunge Kushughulikia Malalamishi kuendesha uchunguzi kuhusu madai ya Bw Muchere.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai.

“Kamati hiyo inatarajiwa kushughulikia ombi hili na kuwasilisha ripoti yake bungeni na kwa mlalamishi kwa mujibu wa Sheria za Bunge,” akasema Spika Wetang’ula.

Kile kinachoibua shauku ni kwamba Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF na mwenyekiti wa bodi ya asasi hiyo katika ripoti zao zilizoandamanishwa na Ripoti na Taarifa ya Kifedha ya Mwaka wa Kifedha wa 2021/2022, “walikosa kutaja au kuelezea misingi ya malipo hayo feki.”