NHIF yapunguza pesa za dialisisi, CT-Scan

NHIF yapunguza pesa za dialisisi, CT-Scan

JOHN MUTUA na GERALD ANDAE

WAKENYA wanaotegemea Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kuwalipia bili za hospitali, sasa watagharimika zaidi.

Hii ni baada ya NHIF kupunguza kiwango cha pesa inazowalipia wagonjwa wanaopokea huduma za usafishaji wa figo (dialysis) na ukaguzi wa maungo ya mwili kupitia MRI na CT-Scan.

Kulingana na mpango huo, NHIF itakuwa ikilipia dialisisi Sh6,000 kutoka Sh9,500 inazolipa sasa; MRI itapungua hadi Sh9,600 kutoka Sh15,000; nao wanaopigwa picha za CT-Scan watalipiwa Sh6,000 kutoka Sh8,000.

Hazina ilisema imechukua hatua hiyo katika juhudi za kupunguza gharama za matumizi, ambazo zimepanda hadi Sh2.7 bilioni kila wiki.

Hata hivyo, NHIF imeongeza pesa inazolipia wanaougua saratani.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF, Bw Peter Kamunyo, watu wengi wanaougua maradhi sugu yasiyo na tiba wamekuwa wakijiandikisha kujiunga na hazina hiyo baada ya kugunduliwa kuwa na maradhi hayo.

Kwingineko, kampuni 30 za kutengeneza vyakula vya mifugo zimefungwa kutokana na uhaba wa mali ghafi.

Kufungwa kwa viwanda hivyo kumesababisha wafanyakazi kupoteza ajira pamoja na kupanda kwa bei ya lishe hizo za mifugo.

Kwa mujibu wa Chama cha Watengenezaji Lishe ya Mifugo (Akefema), kumekuwa na uhaba mkubwa wa maharagwe aina ya soya pamoja na mbegu za alizeti – ambazo ni viungo muhimu katika utengenezaji wa vyakula hivyo.

Bei ya soya na alizeti imepanda maradufu baada ya taifa la Zambia, ambalo huuzia Kenya kiasi kikubwa cha mazao hayo, kupiga marufuku uuzaji wake nje ya nchi hiyo.

Katika muda wa wiki moja iliyopita, bei ya chakula cha kuku wa kutaga mayai imepanda kutoka Sh3,800 hadi Sh3,100 kwa gunia la kilo 50.

Chakula cha vifaranga wa mayai nacho kinauzwa Sh4,200 ikilinganishwa na bei ya awali ya Sh3,250.Nayo bei ya chakula cha ng’ombe wa maziwa imepanda kutoka Sh2,500 hadi Sh3,400 kwa gunia la kilo 70.

Kupanda kwa bei hizo kumelazimisha wafugaji kupunguza matumizi yake, hali ambayo ina athari kwa uzalishaji wa maziwa, mayai na nyama.

You can share this post!

Viongozi wa Gusii mbioni kuunda chama chao cha siasa

UMBEA: Jinsi unavyoweza kuwasha moto hisia tena hadi...