Michezo

Ni afueni kwa Gor waratibu wa KPL wakipangua gozi

March 21st, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

VINARA wa kampuni ya KPL inayoendesha kampeni za Ligi Kuu ya humu nchini hatimaye wameahirisha mechi iliyokuwa iwakutanishe Gor Mahia na Ulinzi Stars wikendi hii.

“Mechi ya raundi ya 16 ya Ligi Kuu iliyoratibiwa kuwakutanisha Ulinzi na Gor Mahia mnamo Jumamosi ya Machi 23 imepanguliwa,” ikasema sehemu ya taarifa ya KPL.

Hatua hiyo inachochewa na kilio cha kocha Hassan Oktay wa Gor Mahia aliyelalamikia ugumu wa ratiba ya kipute hicho kwa masogora wake ambao pia wanawakilisha Kenya katika soka ya Kombe la Mashirikisho barani Afrika.

Kocha Hassan Oktay wa klabu ya Gor Mahia. Picha/ Maktaba

Mchuano huo uliokuwa utandazwe nje ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ungalishuhudia Gor Mahia wakishuka ugani Afraha, Nakuru bila ya huduma za wachezaji watano wa haiba. Mechi hiyo ambayo awali ilikuwa imeratibiwa kutandazwa mnamo Machi 3, iliahirishwa hadi Machi 6 kabla ya kusogezwa upya ili kupisha kampeni za kimataifa za Kombe la Mashirikisho barani Arika (CAF Confederations Cup) zinazoshirikisha Gor Mahia.

Philemon Otieno, Joash Onyango na Francis Kahata watakuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kitakachotegemewa na kocha Sebastien Migne dhidi ya Ghana jijini Accra mwishoni mwa wiki hii katika kipute cha kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON).

Isitoshe, Francis Mustafa na Jacques Tuyisenge wa Burundi na Rwanda mtawalia, watakuwa wakivalia jezi za mataifa yao katika mechi za kimataifa.

Tarehe mpya

Kwa mujibu wa KPL, tarehe mpya ya kusakatwa kwa mchuano kati ya Ulinzi Stars na Gor Mahia itatolewa mapema wiki ijayo. Kusogezwa kwa mechi hiyo ni afueni kubwa kwa Gor Mahia, Ulinzi Stars na kocha Oktay ambaye awali alikuwa amewachemkia vinara wa KPL kwa kukiuka kalenda ya FIFA.

“Yasikitisha kwamba waendeshaji wa KPL wanaweza kulazimisha klabu kuchuana wakati wa mapumziko wa kimataifa,” akatanguliza Oktay.

“Kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, hakuna mechi zozote za ligi zinazostahili kupigwa wikendi hii. Pili, Gor Mahia tayari ina wachezaji watano watakaokuwa wakivalia jezi za timu mbalimbali za taifa mwishoni mwa wiki hii,” akasema.

Baada ya kumenyana na Tusker FC hapo Jumatano uwanjani Ruaraka, Ulinzi Stars wangeshuka dimbani kupimana ubabe na Gor Mahia kabla ya kuwaalika mabingwa wa 2006 SoNy Sugar mnamo Machi 27.

Ilikuwa na maana kwamba wanajeshi hao wanaonolewa na kocha Dunstan Nyaudo wangalilazimika kutandaza jumla ya mechi tatu chini ya kipindi cha wiki moja.

Kufikia sasa, Gor Mahia ambao wamepiga jumla ya mechi 15 pekee wanajivunia alama 32 huku Ulinzi Stars wakifunga mduara wa 10-bora kwa alama 21 kutokana na mechi 16.

Gor Mahia walikuwa jana wenyeji wa Kenpoly mjini Machakos katika mechi ya kufuzu kwa raundi ya 16-bora ya SportPesa Shield Cup.