Ni aibu Magoha kupotosha kuwa ni rahisi kustawisha nchi ‘ndogo’ kuliko nchi ‘kubwa’

Ni aibu Magoha kupotosha kuwa ni rahisi kustawisha nchi ‘ndogo’ kuliko nchi ‘kubwa’

Na SAMMY WAWERU

RWANDA ni nchi ndogo na iliyopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa serikali ya Mbeberu mwaka wa 1961.

Taifa hilo linalopakana na Uganda, Burundi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), lina ukubwa 26,338 km2.

Aidha, Rwanda inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 12.6.

Ni nchi ndogo ikilinganishwa na Kenya, yenye ukubwa wa 580,367 km2, takwimu za hivi punde za KNBS zikionyesha ina zaidi ya watu milioni 47. Kenya ilipata uhuru 1963.

Matamshi ya hivi majuzi ya Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kwamba “Rwanda ni taifa dogo lisilopaswa kulinganishwa na Jamhuri ya Kenya katika utekelezaji wa maendeleo,” yamezua mdahalo mkali, wakosoaji wakishangaa ni kwa namna gani kiongozi mwenye hadhi ya juu serikalini kurusha matamshi tatanishi.

Waziri Magoha alitoa matamshi hayo wakati akionekana kujibu na kutegua kitendawili cha Rwanda ilivyoweza kutengeneza zaidi ya madarasa 22,000 chini ya kipindi cha mwaka mmoja pekee, ili kufanikisha watoto kurejea shuleni na kuweza kuwa na nafasi ya kutosha kujizuia kuambukizwa virusi hatari vya corona.

Shule zote nchini zilifunguliwa jana Jumatatu, Januari 4, 2021, miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mkurupuko wa Covid-19. Desemba 2020, Rais Kenyatta alisisitiza sharti kila mtoto arejee shuleni.

Kenya ni nchi yenye raslimali za kutosha, na miaka ya 70 uchumi wake na mataifa yaliyoimarika kama Japan na Urusi, ulikuwa katika daraja moja.

Waziri Magoha alisema ukubwa wa Rwanda ni sawa na jimbo moja la Kenya, hivyo basi utekelezaji wa maendeleo si kikwazo.

“Huwezi ukalinganisha Kenya na Rwanda. Mimi si mwanasiasa, ila mgao wa serikali kwa maendeleo hutumika kuimarisha barabara, shule, kati ya miradi mingineyo.

“Si haki kwa vyombo vya habari au yeyote yule kulinganisha Kenya na mataifa mengine. Rwanda ni kama jimbo dogo Kenya,” Waziri huyo wa Elimu akasema mnamo Jumapili usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Ni matamshi yanayoendelea kukosolewa na kutajwa kama kauli ya aibu Magoha kupotosha kuwa ni rahisi kustawisha nchi ‘ndogo’ kuliko nchi ‘kubwa’.

Licha ya changamoto chungu nzima ilizoshuhudia awali, kufuatia vita vya ndani kwa ndani, kati ya Wahutu na Watutsi miaka ya 90, Rwanda imeamka kwa kishindo kimaendeleo.

“Rais Paul Kagame (Rwanda) anafikiria kuhusu kizazi kijacho, ilhali baadhi ya viongozi wenzake Afrika wanapanga watavyojinufaisha kwa sababu ya ulafi na tamaa za ubinafsi,” @Zakari Bukari akachapisha katika Facebook, akionekana kumjibu Waziri Magoha.

“Kenya, viongozi walikuwa ‘kazini’ wakiiba pesa za Covid-19, pengine zitasaidia kutengeneza madarasa,” #Julia Jepleting akaeleza kushangaa kwake.

Wachangiaji wa mitandao wanashangaa kwa nini serikalii iipe kipau mbele Ripoti ya Maridhiano (BBI), badala ya masuala yanayohusu wananchi na wanao.

“Kulingana na Profesa, kufunza chini ya miti ni ubunifu. BBI ndio bora zaidi kuliko watoto wetu,” @Jesse Kiugu akacharura.

Profesa Magoha hata hivyo alisema serikali imejikakamua kuhakikisha watoto wanazuiwa kuambukizwa corona shuleni, akitaja kutenga maski zipatazo milioni 7.5 kama baadhi ya mikakati ya maandalizi.

“Serikali imesimamisha mambo yake kuona shule zinafadhiliwa. Kwa sasa, sekta ya elimu ndiyo inapokea mgao mkubwa wa bajeti, kati ya asilimia 27 – 30,” akaelezea.

Aidha, Waziri huyo wa Elimu pia alisema serikali imesambaza asilimia 60 ya madawati yanayohitajika shuleni.

“Kutokana na hali ilivyo tunatarajia msongamano wa watoto katika shule za umma,” akasema.

Alidokeza kwamba zaidi ya shule 43, 000 zitashuhudia msongamano wa watoto.

Mapema Jumatatu kwenye ziara yake katika shule mbalimbali kutathmini shughuli za ufunguzi, alikiri kuafikia umbali wa mita moja kati ya mwanafunzi na mwenzake itakuwa vigumu.

You can share this post!

Vinara wa KRU wakuna vichwa katika juhudi za kufanikisha...

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu azuru Shule ya Mwiki Githurai