Ni Chelsea na Manchester City kwenye fainali ya UEFA Mei 29

Ni Chelsea na Manchester City kwenye fainali ya UEFA Mei 29

Na MASHIRIKA

CHELSEA watakutana na Manchester City kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 29 baada ya kocha Thomas Tuchel kuwaongoza masogora wake kuwakomoa Real Madrid 2-0 kwenye marudiano ya nusu-fainali uwanjani Stamford Bridge mnamo Jumatano usiku.

Ushindi huo wa Chelsea uliwasaidia kuwadengua Real ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la UEFA kwenye hatua ya nusu-fainali kwa jumla ya mabao 3-1.

Ni mara ya kwanza tangu 2018-19 ambapo Liverpool waliwacharaza Tottenham Hotspur 2-0 ugani Wanda Metropolitano jijini Madrid, Uhispania kwa fainali ya UEFA kukutanisha vikosi vyote viwili vya Uingereza. Fainali ya msimu huu itaandaliwa jijini Istanbul, Uturuki.

Chelsea walimtegemea pakubwa kipa Edouard Mendy aliyemnyima fowadi Karim Benzema nafasi mbili za wazi za kuwafunga Chelsea katika kipindi cha kwanza na cha pili.

Ingawa hivyo, Timo Werner aliwafungulia Chelsea ukurasa wa magoli katika dakika ya 28 baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo mvamizi, Kai Havertz. Bao hilo liliwapa Chelsea motisha ya kujituma zaidi huku wakitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha pili.

Kipa wa zamani wa Chelsea ambaye kwa sasa anawasakatia Real, Thibaut Courtois alishughulishwa vilivyo na wanasoka wa Chelsea wakiwemo N’Golo Kante, Havertz na Mason Mount aliyefunga goli la pili baada ya kukamilisha krosi aliyopokezwa na Christian Pulisic katika dakika ya 85.

Ni mara ya kwanza kwa Chelsea kufika fainali ya UEFA tangu 2012 walipowapiku Bayern Munich kutoka Ujerumani kwa 4-3 kupitia mikwaju ya penalti na kunyanyua ufalme.

Chelsea kwa sasa wameweka hai matumaini ya kocha Tuchel kutia kapuni mataji mawili katika msimu wake wa kwanza kambini mwa kikosi hicho. Mbali na kufukuzia ubingwa wa UEFA, Chelsea wanawania fursa ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora na watavaana na Leicester City kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 15, 2021 ugani Wembley, Uingereza.

Matokeo dhidi ya Real yanaashiria ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa makali ya Chelsea chini ya Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Tuchel kwa sasa ana fursa ya kurekebisha mambo baada ya kilichokuwa kikosi chake, Paris Saint-Germain (PSG) kutoka Ufaransa kupokezwa kichapo cha 1-0 na Bayern kwenye fainali ya msimu uliopita wa 2019-20 jijini Lisbon, Ureno. Kwa upande wao, Man-City walitinga fainali baada ya kuwabandua PSG kwa jumla ya mabao 4-1.

Ingawa Man-City ya kocha Pep Guardiola inapigiwa upatu wa kupepeta Chelsea kwenye fainali ya UEFA, kibarua kilichopo mbele yao si rahisi ikizingatiwa kwamba Chelsea waliwahi kuwapokeza kichapo cha 1-0 kilichowadengua kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kikosi cha Hertha Berlin nchini Ujerumani chamtimua Jens...

Orengo hatatemwa, Raila afafanua