Habari MsetoSiasa

Ni dharura gani ya Huduma Namba iliisukuma serikali?, maseneta washangaa

November 25th, 2019 1 min read

Na IBRAHIM ORUKO

MASENETA sasa wanaitaka serikali ifafanue ni dharura gani iliyochochea msukumo wa kukumbatia usajili wa Huduma Namba na pia ibainishe ni lini itatoa kadi kwa wananchi.

Viongozi hao sasa wanamtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kufika mbele ya seneti na kutoa taarifa kwa nini mchakato wa kutolewa kwa kadi za Huduma Namba umecheleweshwa.

Kwenye mjadala ulioandaliwa Alhamisi wiki jana, maseneta hao walikashifu wizara hiyo kwa kutotoa habari kutoka kwa kampuni ya NIIMS ambayo ilikusanya data za Wakenya wote waliokuwa na umri wa miaka sita na zaidi wakati wa usajili huo.

Baada ya kukusanya data, NIIMS ilifaa kutoa nambari spesheli kwa kila Mkenya ambaye angeitumia kupata huduma mbalimbali za serikali.Kabla ya kuzinduliwa Aprili mwaka huu, Wizara ya Usalama wa Ndani ilitangaza kwamba Huduma Namba ndiyo stakabadhi pekee ambayo ingetumika kuwatambua Wakenya.

Stakabadhi kama kitambulisho, nambari ya KRA, kadi za NSSF na NHIF, leseni ya kuendesha magari na pasipoti hazingetumika tena kwa kuwa nambari hiyo ingetoa maelezo yote ya kila Mkenya ikitumiwa wakati wa utoaji huduma.