Michezo

Ni fainali ya ‘Oga’ kumla ‘Ndovu’ dimba la AFCON

February 8th, 2024 2 min read

ABIDJAN, Cote d’Ivoire

NIGERIA walisherehekea kufika fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11 baada ya kuzima Afrika Kusini kwa njia ya penalti 4-2 katika nusu-fainali ya kwanza Jumatano.

Super Eagles watafufua uhasama wao na Cote d’Ivoire katika fainali baada ya wenyeji hao kunyamazisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 2-1 katika nusu-fainali ya pili.

Mabingwa wa Afcon wa mwaka 1980, 1994 na 2013 – Nigeria- walikamilisha muda wa kawaida na ziada dhidi ya Afrika Kusini kwa kufungana 1-1.

Beki William Troost-Ekong na kiungo Teboho Mokoena waliwamwaga makipa Stanley Nwabili na Ronwen Williams kwa penalti, washambulizi Victor Osimhen na Percy Tau walipoangushwa ndani ya kisanduku katika dakika ya 65 na 90, mtawalia.

Super Eagles ilidhani imepata bao la ushindi katika muda wa kawaida, dakika ya 85, Osimhen aliposukuma wavuni pasi safi kutoka pembeni kulia.

Hata hivyo, VAR ilionyesha kuwa Tau alikuwa amevyogwa ndani ya kisanduku cha Nigeria kabla ya shambulio la Super Eagles.

Bafana Bafana itajilaumu yenyewe kufikiwa na masaibu hayo kwani ilipata nafasi ya wazi dakika za lala salama za muda wa kawaida Nwabili alipotema ikabu ya Mokoena miguuni mwa Khuliso Mudau aliyepiga shuti nje.

Mabingwa wa 1996 Afrika Kusini walipata pigo zikisalia dakika tano muda wa ziada utamatike pale Grant Kekana alionyeshwa kadi nyekundu kwa kucheza visivyo.

Katika upigaji wa penalti kuamua mshindi, Terem Moffi, Kenneth Omeruo, Troost-Ekong na Kelechi Iheanacho walufanga penalti za Nigeria iliyopoteza moja kutoka kwa Ola Aina.

Mihlali Mayambela na Mothobi Mvala walipachika penalti za Afrika Kusini, huku Nwabili akawazima Mokoena na Evidence Makgopa.

Ni mechi iliyohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 50,000 wakiwemo naibu rais wa Nigeria Kashim Shettima na rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe.

Nusu-fainali ya pili pia iliwaniwa vilivyo, huku Elephants wakikanyaga Leopards 1-0 kupitia bao la Sebastien Haller dakika ya 65.

Afrika Kusini na DR Congo zitavaana kutafuta mshindi wa medali ya shaba hapo kesho nao Nigeria na Cote d’Ivoire watapepetana Jumapili. Elephants walipoteza 1-0 dhidi ya Super Eagles walipokutana katika Kundi A mnamo Januari 18.

Mshindi na nambari mbili watatuzwa Sh1.1 bilioni na Sh641.9 milioni, mtawalia. Nambari tatu na nne watatia mfukoni Sh401.2 milioni kila mmoja.