Habari MsetoSiasa

Ni haki yetu kupewa marupurupu, wasema 'waheshimiwa'

May 20th, 2019 2 min read

Na LUCY MKANYIKA

KAMATI ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa imetetea uamuzi wa Tume ya Huduma za Bunge kuidhinisha marupurupu ya nyumba ya wabunge.

Akiongea mjini Wundanyi wakati wa kutoa maoni ya bajeti ya serikali, mwanachama wa kamati hiyo Dkt John Mutunga alisema ni haki yao kupata marupurupu hayo.

Alisema kuwa wafanyikazi wengine wa serikali wana marupurupu mengi kuliko wabunge na hakuna malalamishi yeyote yanayoibuka.

Dkt Mutunga alisema kuwa Tume ya Mishahara na Marupurupu Nchini (SRC) inataka kufitini wabunge na wananchi.

“Marupurupu yetu yalikuwa yamebajetiwa na hamna shida tukiyapokea kwani ni haki yetu,” akasema.

Alisema kuwa SRC ilikosea kuwataka wabunge kurudisha fedha hizo.

Alisema kuwa wabunge wamekuwa wakionewa na kuilaumu SRC kwa kutenga wabunge na wafanyikazi wengine wa umma.

“Hakuna shida yeyote ya wabunge kutetea haki yao. SRC inataka kuonyesha wananchi kuwa sisi tuna ubinafsi na huo si uhalisi wa mambo,” akasema.

Mbunge huyo wa Tigania Magharibi aliwataka wananchi kupigania uharibifu wa mali ya umma serikali haswa katika wizara mbalimbali.

Alisema mawaziri na makatibu hupokea mishahara mikubwa na vilevile marupurupu na magari ya kutembelea.

“Sisi ndio tunaowapiga misasa baadhi ya maafisa hawa lakini hao ndio wanapata mishahara ya juu kutuliko. Hayo hamuoni?” akauliza wananchi waliofika kutoa maoni yao kuhusu bajeti hiyo.

Aidha, mbunge huyo alisema kuwa pesa za mkopo wa nyumba wanazopewa ni haki yao.

“Fedha hizo ni za mkopo na inamaanisha kuwa tutazirudisha,” akasema.

Vilevile, alisema kuwa bajeti hiyo haijaipa kipau mbele bunge licha ya kuwa na majukumu mengi.

Alisema kuwa fedha nyingi zinatengwa kwa serikali ya kitaifa ili kufanya miradi lakini hufujwa kwa ufisadi.

Wenyeji wa kaunti hiyo waliwataka wabunge hao kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika jinsi inavyotakikana.

Mwenyeji mmoja Paul Olin’ga alisema kuwa wananchi wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa kodi huku fedha zikifujwa kwa ufisadi.

“Tunataka mtuambie kwa nini sisi tunateseka tukilipa kodi ilihali nyinyi mnajiongezea marupurupu,” akawauliza wabunge hao.

Wakitoa maoni yao, wenyeji walipendekeza kutekelezwa kwa mradi wa bomba la pili la Mzima.

Vilevile waliitaka serikali kutengeneza barabara haswa ile ya Kishushe-Ndii ambayo hutumiwa kusafirisha madini ya chuma yanayochimbwa katika mgodi wa Kishushe.