Michezo

Ni historia kubwa timu yoyote ya Kenya kubwaga Tunisia, mashabiki wasema Bandari ikibwaga US Ben Guardane

September 14th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wametaja ushindi wa Bandari wa mabao 2-0 ya US Ben Guardane kutoka Tunisia kwenye Kombe la Mashirikisho la Afrika mnamo Jumamosi wa kihistoria kwa timu za Kenya.

Wakitoa maoni yao baada ya mabao ya Yema Mwana na Abdalah Hassan kuzamisha Ben Guardane uwanjani Kasarani, mashabiki wamepongeza mabingwa hao wa Kenya wa Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka nchini wa mwaka 2015 na 2018.

Shabiki Mosoti Elijah amesema, “Kupiga klabu kutoka Tunisia ni kitu kikubwa sana kwetu. Pongezi vijana wetu.”

Mbali na kumiminia Bandari sifa tele, mashabiki pia wametoa ushauri kabla ya mechi ya marudiano wiki mbili zijazo.

Edward Mwangi, “Heko Bandari. Jipangeni vyema kwa mechi ya marudiano ili mumalize kazi ugenini.”

Dee Nick, “Hongera. Sasa, endeni Tunisia na mkamilishe kazi.”

Saleem Islimar, “Tumewashabikia nyumbani na sasa tunataka muende Tunisia kutafuta bao la ugenini.”

Naye Samlim Muhsin anaamini “soka ya Kenya imepiga hatua moja mbele”, huku Brian Lytton akijawa na imani Bandari sasa itafika mechi za makundi.

Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza ilionekana itatamatika bila bao baada ya bao kukosekana kwa zaidi ya saa nzima.

Hata hivyo, vijana wa kocha Bernard Mwalala walijitahidi na kupata mabao mawili ya haraka kupitia kwa Yema Mwana na Abdalah Hassan dakika ya 70 na 75, mtawalia.

Mwana alikamilisha kwa ustadi krosi ya Hassan kupitia kichwa chake kuweka Bandari kabla ya Hassan kuimarisha uongozi huo alipomegewa krosi murwa kutoka kwa William Wadri.

Bandari, ambayo inashiriki soka hii ya daraja ya pili ya Bara Afrika kwa mara ya pili katika historia yake, sasa imejiweka pazuri kuimarisha matokeo yake ya mwaka 2016.

Mwaka 2016, Bandari ililemewa na Saint-Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 2-0 mjini Lubumbashi katika mechi ya mkondo wa kwanza ya awamu ya kuingia raundi ya kwanza. Ilibanduliwa nje katika awamu hiyo baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano uwanjani Nyayo jijini Nairobi.

Katika ziara yake ya pili, Bandari ilitinga raundi ya kwanza kwa kubandua nje Wasudan Al-Ahly Shendi kupitia bao la ugenini baada ya kutoka 0-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza na kulazimisha 1-1 mjini Shendi. Nayo Ben Guerdane ilipepeta Amarat United kwa jumla ya mabao 5-1 yote yaliyokuwa yamepatikana nchini Tunisia.

Inamaanisha Bandari italazimika kuwa makini zaidi ugenini kwa sababu Ben Guerdane itatafuta kutumia uwanja wake wa nyumbani kuhakikisha inalipiza kisasi.

Washindi 16 wa raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho watafuzu kushiriki mechi za muondoano dhidi ya timu 16 zitakazokuwa zimebanduliwa nje kutoka Klabu Bingwa ili kuunda makundi.