Ni kisasi tu wikendi hii!

Ni kisasi tu wikendi hii!

LONDON, Uingereza

Na MASHIRIKA

Viongozi Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City watakuwa mawindoni kulipiza kisasi dhidi ya Manchester United na West Ham mtawalia watakaozuru nyuga za Stamford Bridge na Etihad kwa mechi kubwa za Ligi Kuu (EPL) wikendi hii.

Chelsea ya kocha Thomas Tuchel haina ushindi dhidi ya ‘mashetani wekundu’ wa United uwanjani Bridge tangu ishinde 1-0 kwenye Kombe la FA mnamo Mei 2018. Tangu wakati huo, Chelsea wamekabwa mara mbili ikiwemo ya mwisho walipokutana Februari mwaka huu walipotoka 0-0 ligini na kupoteza kwenye Kombe la FA 2-0 (Februari 2019), katika kipute cha Carabao 2-1 (Oktoba 2019) na 2-0 ligini Februari 2020.

Chelsea itajibwaga uwanjani na motisha tele baada ya kuaibisha miamba wa Italia Juventus 4-0 kupitia magoli ya Trevor Chalobah, Reece James, Callum Hudson-Odoi na Timo Werner kwenye Klabu Bingwa Ulaya hapo Novemba 23.“Blues” pia alikung’uta Leicester 3-0 ligini kupitia mabao ya Antonio Rudiger, N’Golo Kante na Christian Pulisic mnamo Novemba 20 na haijapoteza michuano 10 mfululizo katika mashindano yote.

“Reds” kwa upande wake, ilianza maisha bila kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa kulipua Villarreal 2-0 kupitia mabao ya gunge Cristiano Ronaldo na Jadon Sancho.Solskjaer alitimuliwa kwa msururu wa matokeo duni, huku naibu wake Michael Carrick akitwikwa majukumu ya kuongoza timu kwa muda.

United imehusishwa na kocha Mjerumani Ralf Rangnick.City ya kocha Pep Guardiola imeshinda mechi zake zote nne imesakata mwezi huu ikiwemo kupepeta miamba Manchester United 2-0 ligini na Paris Saint-Germain kwenye Klabu Bingwa Ulaya.

Hata hivyo, ilichapwa na West Ham 1-0 na kubanduliwa kwenye kipute cha Carabao zilipokutana mara ya mwisho jijini London mnamo Oktoba 27. Michuano hiyo inatarajiwa kuwa moto, Chelsea ikilenga kukwamilia uongozi na kudumisha mwanya wa alama tatu dhidi ya nambari mbili City.

West Ham ni ya nne kwa alama 23, mbili nyuma ya nambari tatu Liverpool na tatu nyuma ya City. United, ambayo inapatikana katika nafasi ya nane kwa alama 17, haina pointi kutoka mechi zake mbili zilizopita ligini baada ya kulemewa 4-1 na Watford mnamo Novemba 20. Jumla ya michuano mitano itachezwa leo.

You can share this post!

Ajenti wa Bale achemkia mashabiki wa Real madrid kwa...

Masuala yanayomfanya Mudavadi ‘kuchukia’ Raila

T L