Ni kubaya 2022!

Ni kubaya 2022!

Na WAANDISHI WETU

GHASIA zilizotawala chaguzi ndogo zilizoandaliwa jana zimetoa taswira hatari na ya kutisha huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Matukio hayo ya ghasia yalishuhudiwa kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu na Kabuchai pamoja na wadi za London na Kiamokama katika kaunti za Nakuru na Kisii mtawalia.

Kiini cha machafuko hayo kilikuwa madai ya baadhi ya wabunge kutoa hongo kwa wapigakura na maafisa wa uchaguzi kudaiwa kuwapendelea baadhi ya wawaniaji.

Hasa yalihusisha wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga kwa upande mmoja na wandani wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kwa upande mwingine.

Kilele cha ghasia hizo kilikuwa katika eneobunge la Matungu ambapo aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa alimzaba kofi afisa wa uchaguzi katika kituo cha kupiga kura shuleni Bulonga Primary.

Bw Echesa ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto na aliyekuwa akimpigia upato mwaniaji wa chama cha UDA, Bw Alex Lanya, alinaswa akimkaripia afisa huyo wa uchaguzi kisha kujibizana naye kabla ya kumzaba kofi.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Bonny Khalwale walikwepo wakati wa ghasia hizo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati tayari amezitaka idara za usalama kumkamata Bw Echesa ili achukuliwe hatua za kisheria.

“Uvamizi huo haukufaa na ninawaomba maafisa wa polisi wafuatilie suala hilo na kumkamata waziri huyo wa zamani ili awajibikie matendo yake,” Bw Chebukati akawaeleza wanahabari mjini Naivasha.

Mwakilishi wa Kike, Bi Elsie Muhanda naye alilazimika kunusuru maisha yake kwa kutimua mbio baada ya makundi ya vijana kumvamia na kulipiga mawe gari lake huku wengine wakijaribu kutoa pumzi kwenye magurudumu ya gari hilo.

Bi Muhanda ambaye anahudumu kupitia chama cha ODM alidai kuwa vijana hao walitumwa na Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala.

Hali ilikuwa hiyo hiyo katika eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma ambako wabunge Didmus Barasa (Kimilili), Nelson Koech (Belgut), Wilson Kogo (Chesumei) na Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei walikamatwa baada ya jembe na silaha butu kupatikana kwenye moja ya magari yaliyokuwa katika msafara wao kwenye soko la Chwele.

Wandani wa Dkt Ruto nao walifurushwa na vijana wenye hamaki katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya msingi ya Milimani, Wadi ya London, Nakuru.

Gari la mbunge wa Lang’ata, Bw Nixon Korir lilipigwa mawe na kuharibiwa vibaya huku wanahabari watatu pia wakijeruhiwa kwenye purkushani hizo.

Bw Korir, maseneta Susan Kihika (Nakuru), Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na mbunge wa Emurua Dikir, Bw Johanna Ng’eno walitimuliwa kwa nguvu kutoka kituoni humo baada ya kurushiwa vitoa machozi na maafisa wa usalama.

Mwaniaji wa UDA katika Wadi ya Kiamokama, Bw Nyandusi Nyakeramba alinyakwa pamoja na mfanyabiashara Bosco Gichana kutokana na ghasia zilizozuka katika eneo la Moremani, Kisii.

Ripoti za Cecil Odongo, Shabaan Makokha, Onyango K’Onyango na Wycliffe Nyaberi

You can share this post!

Echesa akamatwe – Mutyambai

Wazee Kisumu wataka serikali iwarejeshee joka lao la Omieri