Michezo

NI KUBAYA! Arsenal iko pabaya Ligi ya Uropa

March 9th, 2019 2 min read

RENNES, Ufaransa

ARSENAL inakodolea macho kuaga soka ya Ligi ya Uropa baada ya kuduwazwa 3-1 na Rennes katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya 16-bora Alhamisi.

Huku Chelsea na Napoli zikinusia kuingia robo-fainali baada ya kukanyaga Dynamo Kiev na Salzburg bila huruma 3-0, Arsenal sasa inakabiliwa na kibarua kigumu kusalia mashindanoni.

Alex Iwobi aliipa Arsenal uongozi dakika ya tatu uwanjani Roazhon Park, lakini Rennes ikapata nguvu kubadilisha mkondo wa mechi baada ya beki Sokratis Papastathopoulos kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 41.

Benjamin Bourigeaud alisawazisha 1-1 dakika ya 42 kabla ya wenyeji Rennes kuongeza mabao mawili katika kipindi cha pili pale ilipowekea Arsenal presha kali.

Nacho Monreal alifungia Rennes bao la pili alipocheka na nyavu za timu yake dakika ya 65 kabla ya Ismaila Sarr kugonga msumari wa mwisho dakika ya 88.

Vijana wa Unai Emery lazima washinde mechi ya marudiano 2-0 jijini London juma lijalo kusalia katika mashindano haya ambayo pia ndiyo nafasi yao ya pekee ya kushinda taji msimu huu.

Ubingwa wa Ligi ya Uropa utawapa Arsenal, ambao wako nje ya mduara wa nne-bora kwenye Ligi Kuu, tiketi ya kurejea katika Klabu Bingwa baada ya kukosa makala mawili yaliyopita.

“Nadhani tunaweza kufanya vizuri zaidi, kichapo cha mabao 3-1 ni kikali kwetu,” alikiri Emery.

“Tutawazia mchuano huu kwa wiki nzima. Tutaanza mechi ya marudiano wachezaji 11 dhidi ya 11, bila Sokratis, bila (Alexandre) Lacazette, lakini tukisakata mechi tulivyofanya katika dakika 40 za kwanza, tukipata msukumo kutoka kwa mashabiki wetu wa nyumbani pia, tutakuwa na uwezo wa kufufua ndoto yetu.”

Arsenal ilipata tiketi ya kukutana na Rennes baada ya kufuta kichapo kutoka mkondo wa kwanza dhidi ya BATE Borisov, lakini Rennes wako hatua moja mbele kimchezo na wanafurahia msimu wao bora kabisa katika mashindano ya Bara Ulaya.

Petr Cech, ambaye alikuwa anakutana na waajiri wake wa zamani Rennes, aliondosha hatari mara kadhaa baada ya Bourigeaud kuweka Wafaransa hao kifua mbele kabla ya Monreal kujifunga naye Sarr akafunga bao la tatu linalotarajiwa kuipa Arsenal kazi ngumu.

Chelsea, ambayo pia huenda ikahitaji kushinda Ligi ya Uropa kurejea katika Klabu Bingwa msimu ujao, ilizamisha Dynamo Kiev kupitia mabao ya Pedro Rodriguez, Willian na Callum Hudson-Odoi uwanjani Stamford Bridge.

Waajiri wa zamani wa Sarri, Napoli walijiweka pazuri kuendelea mashindano walipopapura Salzburg kupitia mabao ya Arkadiusz Milik na Fabian Ruiz, na Jerome Onguene, ambaye alijifunga.

 

Matokeo (Machi 7): Eintracht 0 Inter 0, Sevilla 2 Slavia Prague 2, Zenit 1 Villarreal 3, Rennes 3 Arsenal 1, Dinamo Zagreb 1 Benfica 0, Valencia 2 Krasnodar 1, Napoli 3 Salzburg 0, Chelsea 3 Dynamo Kiev 0.