Habari

Ni kubaya lakini msinilaumu – Uhuru

November 17th, 2019 2 min read

Na GAKUU MATHENGE na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta amekiri kwamba hali si shwari katika utawala wake lakini akajiondolea lawama kuhusu hali hii.

Wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia hali mbaya ya uchumi ambayo imefanya maisha kuwa magumu hasa katika sekta za biashara na kilimo.

Alipozungumza Ijumaa wakati wa mkutano wake na viongozi wa Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, Rais alisema ni kweli kuna mambo mengi ambayo yamemwendea segemnege kinyume na alivyotarajia kiasi cha kutatiza utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Rais alionekana kuwalaumu mawaziri na wabunge kwa hali hiyo, akisema viongozi husika hawajawahi kumwambia kuhusu changamoto zilizopo.

Ilibainika kuwa katika mkutano huo wa faraghani, baadhi ya viongozi walimwambia Rais kuhusu matatizo yanayokumba wananchi hasa wale wa Mlima Kenya waliompigia kura kwa wingi.

“Ninashukuru viongozi kwa kuleta maswala haya ambayo sote tulichaguliwa kutatua kwa niaba ya wananchi. Hata hivyo, haya mambo yote ambayo yamewasilishwa hapa hayajawahi kufikishwa kwangu. Badala yake, ninachosikia katika runinga, televisheni na mitandao ya kijamii ni matusi na hadithi kuhusu uchaguzi wa 2022. Hawajaniletea sheria wala sera zinazohitajika kubadili hali,” akasema Raia Kenyatta.

Katika sekta ya kibiashara, kumekuwa na malalamishi kwamba utawala wa Jubilee ulibuni sera kali zinazotatiza uwekezaji na ujasiriamali. Wataalamu wa masuala ya kiuchumi husema hii imechangia makampuni mengi na viwanda kufilisika au kulazimika kuhamia mataifa ya nje, huku biashara ndogo ndogo pia zikifungwa kwa wingi.

Kwa upande mwingine, sekta ya kilimo imeathirika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo bei ya juu ya pembejeo na uagizaji bidhaa za kilimo kwa bei ya chini kutoka nchi za nje kama vile Uganda na China.

Wakulima ambao wametatizika zaidi katika miaka ya hivi majuzi ni wa kahawa, majani chai na miwa, huku wafugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa pia wakilia kuhusu hasara wanazopata.

Ubwete

Katika hotuba yake, Rais alionekana kuwalaumu mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo na Ufugaji) na Peter Munya (Biashara) bila kuwataja kwa kuzembea katika majukumu yao licha ya kuwa wao pia ni viongozi kutoka Mlima Kenya.

“Tazameni tu muone wale watu ambao nimewapa majukumu ya kutatua mambo haya,” akasema.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria alipozungumza na wanahabari baada ya mkutano huo, alisema hakutakuwa na faida yoyote kama viongozi wataendelea kulaumiana.

Kulingana naye, masuala yaliyojadiliwa Sagana yalikuwa yamewahi kujadiliwa katika mkutano mwingine uliofanywa hapo 2016 lakini hakuna hatua zilichukuliwa.

“Hatutaki kumlaumu Rais kwa lolote lakini pia hatutaki alaumu magavana wala wabunge. Yale tuliyosema hapa 2016 ndiyo yamerudiwa tena leo. Utadhani kuna watu watatoka sayari ya Mirihi (Mars) kutatua shida hizi. Tunataka vitendo,” akasema Bw Kuria.

Hata hivyo, mbunge huyo alitaka pia mawaziri wawajibike kwa kuwa Rais aliwapa kazi akiamini watamsaidia kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi.