Michezo

NI KUBAYA: Sheffield United yatafuna Arsenal

October 23rd, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

SHEFFIELD United waliandikisha ushindi muhimu dhidi ya Arsenal ugani Bramall Lane na kupanda hadi ndani ya mduara wa 10 bora katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Lys Mousset ambaye al;ikuwa akiichezea Sheffield kwa mara ya kwanza alifunga bao la pekee baada ya kuunganisha kona ya Jack O’Connell’s katika kipindi cha kwanza.

Awali, mshambiliaji chipukizi Nicolas Pepe wa Arsenal aliyesaliwa kwa kitita cha Sh9.3 bilioni msimu huu, alipoteza nafasi ya wazi ya kuwaweka waajiri wake kifua mbele licha ya kusalia pekee na kipa wa Sheffield Dean Henderson karibu na lango.

Ushindi huo wa Jumatatu usiku ulikuwa wa kwanza mkubwa kwa Sheffield United tangu warejee ligini, na sasa wanakamata nafasi ya tisa, kwa mwanya wa pointi saba kutoka mahali shoka la kuteremka.

Kwa Arsenal, matokeo hayo yamewanyima fursa ya kutoza kwa nne bora, na sasa wanakamata nafasi ya tano jedwalini, pointi mbili nyuma ya Chelsea wanaokamata nafasi ya nne.

Sheffield wameibukia kuwa timu ngumu kwa vigogo kwenye ligi hii inayojumuisha timu 20, tangu waagane kwa sare ya 2-2 na Chelsea mwezi Agosti, kabla ya kusumbua Liverpool hadi dakika ya mwisho kabla ya kupoteza mechi hiyo kwa 1-0 mwishoni mwa mwezi uliopita.

Dhidi ya Arsenal, walicheza kwa uelewano mkubwa huku McGoldrick akishirikian vyema na Mousset huku wakiiweka safu ya ulinzi ya Arsenal kwenye presha kubwa.

Kocha wao, Chris Wilder aliifanyia mabadiliko madogo kikosi chake kwa kuwapa makinda kadhaa nafasi waonyeshe uwezo wao.

Sheffield haijapoteza mechi yotote tangu 2014 ikiwa uongozini kufikia wakati wa mapumziko kutokana ukuta mkali wa mabeki O’Connel, Chris Basham na John Egan.

“Tutajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi nyingi, hasa katika kipindi cha kwanza,” alisema kocha Unai Emery.

Katika mechi ijayo ya EPL, Arsenal wanakutana na Crystal Palace kwenye mechi ambayo lazima Unai Emery atafute ushindi, la si hivyo huenda akamwaga unga siku hiyo.