Michezo

NI KUBAYA: Utepetevu kikosini Arsenal

October 29th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

HUENDA kipindi cha ukufunzi wa Unai Emery kambini Arsenal kikakosa kudumu kwa muda mrefu iwapo Mhispania huyu hatajinyanyua punde na kurejesha hadhi iliyojivuniwa awali na miamba hao wa soka ya Uingereza.

Hasira ndicho kitu kikubwa kilichohanikiza anga ya uwanja wa Emirates wikendi iliyopita baada ya utepetevu wa masogora wa Emery kuwaruhusu Crystal Palace kutoka nyuma mabao mawili na kusajili sare ya 2-2.

Ni mchuano ambao mwisho wake ulimshuhudia nahodha Granit Xhaka wa Arsenal akiashiria kufadhaika, kukereka na kutamauka baada ya kuondoka uwanjani huku akizomewa na mashabiki.

Kingine ambacho kinazidi kuchemsha hasira ya mashabiki wa Arsenal ni kukosekana kwa mwamko mpya wala ishara za ufufuo wa makali ya kikosi hicho ambacho hakijabadilisha kabisa mtindo wa kucheza kwao tangu kutimuliwa kwa mkufunzi Arsene Wenger mwishoni mwa msimu wa 2017-18.

“Xhaka alikosea sana kwa tendo la kuanika mseto wa hisia za hasira na kutamauka. Maadamu ndiye nahodha, anatazamiwa kuwa mtulivu na kuonyesha sifa za uongozi,” akasema Emery kwa kuahidi kwamba atalazimika kuandaa kikao cha dharura na masogora wake kabla ya kushuka dimbani hapo kesho kwa mchuano wa Carabao Cup dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.

Habari za kuondolewa kwa Xhaka uwanjani zililakiwa na mashabiki kwa wingi wa vifijo na shangwe za kinaya, jambo lililomchochea kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 kuvua shati, kuziba masikio na kujitoma katika chumba cha kubadilishia nguo.

Ilikuwa ni mara ya pili kwa Xhaka ambaye ni mzawa wa Uswisi kuzomewa peupe na mashabiki wa Arsenal msimu huu baada ya kulaumiwa pia kwa matokeo duni dhidi ya Aston Villa mwezi uliopita.

Kuteuliwa kwa Xhaka kuwa nahodha wa Arsenal kulichangiwa kwa ulazima wa kujazwa kwa nafasi ya Mfaransa Laurent Koscielny aliyeingia katika sajili rasmi ya Bordeaux mwishoni mwa msimu uliopita.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano katika jedwali la EPL kwa alama 16, nne zaidi nyuma ya Leicester City na Chelsea wanaousoma mgongo wa Manchester City ambao wanasalia na pointi sita zaidi kuwafikia Liverpool wanaojivunia alama 28.

Katika jumla ya mechi 10 zilizopita, Arsenal wamesajili ushindi mara nne, kutoka sare mara nne na kupoteza mechi mbili. Ni matokeo ambayo kwa sasa yanawaweka katika hatari ya kupitwa na Crystal Palace, Manchester United, Sheffield United, Bournemouth na West Ham United iwapo watang’atwa na Wolves mwishoni mwa wiki hii uwanjani Emirates.

Akihojiwa na wanahabari mwishoni mwa mechi kati ya Arsenal na Palace, Emery pia alifichua kwamba hatua ya kutowajibishwa kwa Mesut Ozil katika mingi ya michuano ya tangu mwishoni mwa msimu uliopita ni uamuzi wa kimakusudi wa usimamizi wa Arsenal.

Ozil, 31, anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na mojawapo ya klabu za Major League Soccer (MLS) nchini Amerika. Kufikia sasa, sogora huyo mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani amechezeshwa mara nne pekee msimu huu na dalili zote zinaashiria kwamba hayupo kabisa katika mawazo ya Emery wala katika mipango ya baadaye ya waajiri wake wa sasa.

Akiwa miongoni mwa wachezaji wanaojivunia kuhudumu kambini mwa Arsenal kwa kipindi kirefu zaidi, Ozil ambaye pia amewahi kuchezea Real Madrid ya Uhispania pamoja na Werder Bremen na Schalke za Ujerumani, aliingia katika sajili rasmi ya Arsenal mnamo 2013.

Tetesi zinamhusisha na uwezekano wa kutua kambini mwa DC United au Inter Miami zinazoshiriki kipute cha Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.