Habari

Ni kubaya!

October 6th, 2019 4 min read

Na VALENTINE OBARA na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameingiwa na wasiwasi tele kuhusu watakavyojikimu kimaisha kutokana na idadi kubwa ya kampuni zinazoendelea kufungwa zikilalamikia sera duni za serikali.

Hali hii imeathiri sekta zote na inatilia shaka mustakabali wa uchumi wa nchi.

Idadi ya kampuni za kibinafsi zinazofungwa au kuvunjwa kwa kushindwa kuhimili mazingira ya kiuchumi imeongezeka maradufu.

Takwimu katika afisi ya msajili wa kampuni zinaonyesha kuwa, kampuni 388 za kibinafsi zimefungwa au kuhama Kenya katika kipindi cha miezi sita kufikia Septamba 21, mwaka huu.

Hali ni mbaya hivi kwamba, katika kipindi cha miezi kumi na sita, zaidi ya kampuni kumi, zikiwemo za kimataifa na za humu nchini zimefuta wafanyakazi baada ya kupata hasara.

Kampuni ya East African Breweries iliwafuta wafanyakazi 100 huku ile ya kutengeneza simiti ya East African Portland ikitangaza kuwaachisha kazi wafanyakazi wote zaidi ya 1,000.

Shirika la Ndege la Kenya ambalo limekuwa likipata hasara ya mabilioni ya pesa liliwafuta wafanyakazi 38.

Katika sekta ya fedha, benki ya Stanbic iliwastaafisha mapema wafanyakazi 200 nayo kampuni ya Finlays iliyobobea katika ukuzaji wa majanichai na maua ikiwatimua wafanyakazi 1,700 mwaka 2018.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kiuchumi, hali hii inatokana na sera za serikali ambazo zimefanya uwezo wa kiuchumi wa Wakenya kudorora.

Kampuni nyingine ambazo zilifunga na kuacha maelfu ya Wakenya bila kazi ni Deacons Limited. Nayo Nestle Foods ilifunga afisi yake jijini Nairobi, hatua ambayo iliathiri wafanyakazi wake 100.

Vile vile, sekta zinazotegemewa na wananchi kujiajiri zinaendelea kukumbwa na misukosuko tele inayofanya wajasiriamali kufunga biashara zao kwa sababu ya hasara wanazopata.

Inahofiwa hali hii huenda ikazorotesha zaidi uchumi wa kitaifa kwani bila mapato, wananchi hawatakuwa na uwezo wa kugharamia mahitaji yao muhimu na hivyo basi biashara tele zitaathirika.

Kwa wiki chache zilizopita, sekta ya kilimo ambayo imekuwa ikisifiwa kuwa kitega uchumi kikuu cha taifa imepitia changamoto tele zinazotia hofu wadau.

Wakulima wa majani chai na kahawa walishtushwa na matangazo ya mashirika yanayosimamia shughuli zao kwamba, faida watakazopata zitapungua kwa kiasi kikubwa mwaka huu.

Ingawa sababu zilizotolewa ni kuwa ushindani wa uzalishaji mazao hayo kimataifa ulizidi, swala ibuka ni kwa nini wakulima wa humu nchini hawakuwezeshwa kufaidika katika ushindani huo ilhali serikali hujisifu kuhusu inavyopiga jeki sekta hii.

Hali sawa na hiyo imo katika kilimo cha miwa na mahindi ambapo masaibu ya wakulima yanaongezeka kila kukicha.

Kampuni zawekwa chini ya mrasimu

Wiki iliyopita, matumaini ya kufufua sekta ya miwa yalididimia wakati usimamizi wa kiwanda kikubwa zaidi cha sukari cha Mumias ulipotwaliwa na Benki ya KCB kwa kushindwa kulipa madeni yake.

Kampuni nyingine iliyowekwa kwenye usimamizi wa mrasimu ni Athi River Mining ambayo ilikuwa ikiajiri maelfu ya wafanyakazi, nayo Telkom Kenya ikafuta asilimia 72 ya wafanyakazi wake.

Unilever Tea Kenya iliwasimamisha wafanyakazi vibarua 11,000 kuanzia mwaka 2018.

Wiki jana, kampuni kubwa za michezo ya bahati nasibu za Sportpesa na Betin ziliamua kufunga biashara zao nchini kwa sababu ya mizozo iliyodumu kwa muda kati yao na serikali kuhusu madai ya kukwepa kulipa ushuru.

Kampuni ya Sportpesa pekee iliwafuta kazi wafanyakazi 400 na kusitisha ufadhili wa miradi mbali mbali ambayo vijana walitegemea kujiajiri ikiwa ni pamoja na spoti.

Betin ilikuwa imefungulia maelfu ya vijana nafasi za kujiajiri kupitia maduka yake kote nchini.

Athari za hatua hiyo ni vijana hao kukosa ajira, wachezaji wa vilabu vikubwa vya michezo vilivyofadhiliwa na kampuni hizo kukosa kupata mishahara na marupurupu yao.

Wakuu wa kampuni hizo walisema mandhari ya kibiashara yamekuwa mabaya mno nchini kwa hivyo ni vigumu kufaidika kibiashara.

Viwanda vya utengenezaji pombe na sigara navyo viliashiria uwezekano wao kufunga biashara zao nchini au kufuta kazi baadhi ya waajiriwa wao, kwa sababu hizo hizo.

Ilani iliyotolewa na mashirika ya British American Tobacco (BAT), Kenya Wine Agencies (Kwal), Alcoholic Beverages Association of Kenya (Abak) na Mastermind Tobacco ilionya kwamba, sera za ushuru zisiporekebishwa, kutakuwa na athari kubwa kwa ajira kwani maduka na kampuni za usambazaji bidhaa zao zitaathirika.

“Italemaza sekta ya kiviwanda na kuathiri hali ya maisha kwa maelfu ya Wakenya,” mashirika hayo yakasema kwenye taarifa ya pamoja.

Katika Kaunti ya Mombasa, wakazi, wanasiasa, mashirika ya kijamii na wakurugenzi wa kampuni za uchukuzi mizigo wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa sasa wakilalamikia jinsi uchumi ulivyodorora tangu serikali ilipoagiza mizigo isafirishwe kwa reli ya kisasa ya SGR.

Imebainika kwamba hatua hiyo haikuathiri wakazi wa Mombasa waliotegemea ajira katika kampuni za uchukuzi wa malori pekee, bali pia Wakenya wengine waliofanya biashara katika barabara ambazo lori hizo zilikuwa zikipitia kama vile Mtito Andei.

“Wakazi wengi wanashindwa hata kulipa kodi ya nyumba. Nyumba zinabaki tupu bila wapangaji kwani wengi wameamua kuhamia miji mingine,” Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema majuzi.

Mjini Kisumu, mamia ya wakazi wanahangaika baada ya maeneo yao ya biashara kubomolewa kiholela serikali ikijiandaa kufanyia ukarabati bandari ya Ziwa Victoria kwa haraka.

Nafasi za ajira zimepotezwa pia katika sekta ya maduka ya jumla baada ya kampuni kadhaa kama vile Choppies na Nakumatt kufungwa.

Kampuni ya Nakumatt ililazimika kuwafuta kazi wafanyakazi 800 huku kuporomoka kwake kukiathiri maelfu ya wafanyabiashara waliokuwa wakiitegemea.

Kampuni za kimataifa ambazo zilihama Kenya zikilalamikia mazingira magumu ya kibiashara ni benki ya Hong Kong Shanghai Banking Corporation (HSBC), Reckitt & Benkiser, Procter & Gamble, Bridgestone, Colgate Palmolive na Johnson & ?Johnson.

“Kinachotendeka ni hatari kwa Kenya kama nchi na kama mbabe wa uchumi Afrika Mashariki. Tunapaswa kulinda himaya yetu ya kibiashara kwa kuwapa motisha wawekezaji wa humu nchini na kimataifa,” asema mwanauchumi Solomon Njoroge.

Anasema kufungwa kwa viwanda na makampuni kunapunguza uwezo wa uchumi wa nchi.

“Serikali ikikosa kuweka mazingira ya kukuza biashara zilizopo na zile mpya, basi nchi itapoteza nafasi yake ya kuwa na uchumi thabati eneo hili,” asema.

Wadadisi wanasema itakuwa vigumu kwa serikali kushawishi Wakenya kwamba, uchumi unakua wanapopoteza kazi.

“Watu wanashangaa serikali inaposema mambo yako shwari wakati maelfu ya watu wanapoteza kazi kampuni zikifungwa na wafanyabiashara kuchelea kuwekeza Kenya kwa sababu ya sera za serikali,” anasema mtaalamu wa masuala ya uchumi David Kimotho.