Michezo

Ni kufa kupona Barcelona wakialika Atletico Madrid

June 30th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ITAKUWA ni kufa-kupona kwa Barcelona leo Jumanne usiku watakaposhuka ugani Camp Nou kupepetana na Atletico Madrid katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) ambao wana ulazima wa kusajili ushindi ili kuweka hai matumaini finyu ya kutetea ufalme wa msimu huu.

Chini ya kocha Quique Setien, Barcelona wamesuasua tangu kurejelewa kwa soka ya Uhispania msimu huu na sare ya 2-2 dhidi ya Celta Vigo mnamo Juni 27, 2020, iliwatikisa hata zaidi.

Matokeo hayo yalishuhudia masogora wa Setien wakipitwa na washindani wao wakuu, Real Madrid ambao kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali kwa alama 71, mbili zaidi Barcelona wanaoshikilia nafasi ya pili.

Zikiwa zimesalia mechi sita pekee kabla ya muhula huu kutamatika rasmi, Real wanahitaji kusajili ushindi katika kila mojawapo au angalau kutia kibindoni alama 16 ili kuwapiga kumbo Barcelona.

Kinyume na Barcelona, Real wameibuka na ushindi katika michuano yao yote mitano tangu kurejelewa kwa kampeni za La Liga zilizosimamishwa mnamo Machi 2020 kutokana na janga la corona.

Wanapojizatiti kuvaana na Atletico ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 58, Barcelona tayari wamepigwa jeki na marejeo ya kiungo Sergio Busquets ambaye amekuwa akitumikia marufuku huku beki Sergi Roberto akipona jeraha.

Fowadi Antoine Griezmann aliyepangwa katika kikosi cha wachezaji wa akiba dhidi ya Celta Vigo katika mechi iliyopita anatarajiwa kurejea leo na kushirikiana vilivyo na Luis Suarez na nahodha Lionel Messi katika safu ya ushambuliaji.

Mechi hiyo itakuwa jukwaa mwafaka zaidi kwa Mesii kutafuta bao lake la 700 katika taaluma ya usakataji wa soka kwenye ngazi ya klabu na timu ya taifa ya Argentina.

Licha ya wachezaji Mario Hermoso na Sime Vrsaljko kuuguza majeraha, kocha Diego Simeone wa Atletico anajivunia kikosi thabiti ambacho ameapa kitawatoa jasho Barcelona watakaokuwa wakichezea nyumbani.

Tangu walazimishiwe sare ya 1-1 kutoka kwa Athletic Bilbao mnamo Juni 14, 2020, Atletico walijinyanyua na kusajili ushindi katika mechi nne zilizofuata.

Ni Real pekee ndio wamepoteza mechi chache zaidi kuliko Atletico msimu huu, ila sare 13 ambazo zimepigwa na wanasoka hao wa Simeone ndizo zinawaponza. Kwa sasa ni pengo la alama 13 ndilo linalowatenganisha na Real wanaonolewa na kocha Zinedine Zidane.

Ingawa Barcelona wangali na fursa ya kujitwalia ubingwa wa La Liga kwa msimu wa tatu mtawalia, kikosi hicho kimepoteza alama 25 ugenini na mbili pekee kutokana na michuano ya nyumbani.

Kocha msaidizi wa Barcelona, Eder Sarabia amekiri kwamba kikubwa zaidi kinachovuruga Barcelona na kutofautiana kwa wachezaji na kocha Setien ambaye kwa sasa haonani uso kwa macho na baadhi ya masogora.