Michezo

Ni kujituma kulitusaidia, si ubunifu – Wenger

April 8th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger anahisi kuwa ushindi wa vijana wake wa 3-2 dhidi ya Southampton Jumapili ulitokana na kujituma zaidi kuliko ubunifu baada ya straika Danny Welbeck kuisaidi timu hiyo kuzoa alama zote tatu wakati matokeo yakiwa  2-2, ugani Emirates.

Baada ya kuiangamiza CSKA Moscow Alhamisi 4-1, na kushinda mkondo wa kwanza wa kipute cha Europa, Arsenal ilijitahidi sana kuipapura timu ambayo tayari imo katika eneo hatari la kuaga ligi kuu ya Uingereza.

Welbeck alitia kimiani bao la kichwa katika dakika ya 81 na kuipa Arsenal ushindi wa sita mfululizo katika mashiondano yote, ingawa Wenger alikiri kuwa uchovu ulichangia pakubwa kwa timu yake kutoonyesha makali yake na kuinyima Southampton nafasi ya kufunga bao.

Hata hivyo, Jack Stephens wa Southampton na Mohamed Elneny wa Arsenal wote walilishwa kadi nyekundu mechi ikikaribia kutamatika kwa uzushi.

Ninaamini ukicheza kila baada ya siku tatu ni vigumu kupata kasi ya mechi,” Wenger aliambia Sky Sports.

“Ukiitazama mechi leo, mara mbili tulikuwa wakati mgumu- mwanzo  tulikuwa 1-0 nyuma kisha wakaja wakafunga tena na kuwa 2-2. Hapo ilitulazimu kusaka mbinu za kushinda mechi.”

“Baadaye mpira ulitutoka kwa mguu na kututisha. Lakini kama tuna vifaa na moyo ya kujituma, hasa wakati mpinzani anamiliki mpira, basi una nafasi,” akasema.