Ni kuni na makaa baada ya bei ya gesi kupanda

Ni kuni na makaa baada ya bei ya gesi kupanda

 Na BARNABAS BII

WAKAZI wa Bonde la Ufa wamekumbatia tena matumizi ya kuni na makaa baada ya bei ya gesi kupanda.

Wauzaji wa gesi sasa wanauza mtungi wa kilo 13 kwa Sh3,200 kutoka Sh2,700. Mtungi wa gesi ya kilo sita unauzwa kwa Sh1,520 kutoka Sh700.

“Bei ya gesi imekuwa ghali na hatuwezi kumudu, ni heri tutumie kuni na makaa kupika,” akasema Bi Veronica Cheptoo, mkazi wa mtaa wa Mwanzo, mjini Eldoret.

Bei ya makaa pia imepanda kutoka Sh1,500 hadi Sh1,800 kutokana na ongezeko la wateja.

Bei ya miti ya mbao pia imeongezeka kutoka Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa kila tani hivyo kuwaletea mapato ya juu wakulima wanaokuza misitu ya kibinafsi.

Hatua ya serikali kupiga marufuku ukataji wa miti katika misitu ya serikali na kijamii miaka minne iliyopita pia imesababisha bei ya kuni na miti kupanda.

Ripoti ya Shirika la Misitu nchini (KFS) inaonyesha kuwa, marufuku hiyo imesababisha serikali kupoteza mapato ya Sh4 bilioni ndani ya kipindi hicho na watu 44,000 wamepoteza kazi.Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (Kefri) unaonyesha kuwa, marufuku hiyo imefanya Kenya kuagiza miti ya mbao kutoka ughaibuni.

“Bei ya miti ya mbao imeongezeka kwa asilimia 22, kuni asilimia 25 na makaa asilimia 40,” alisema Mkurugenzi wa Kefri Joshua Cheboiwo.

Aliambia Taifa Leo kuwa, marufuku ya kukata miti katika misitu ya umma na kijamii ilisababisha kufungwa kwa afisi za shirika hilo katika eneo la Maji Mazuri, Mau Summit, Elburgon, Molo, Makutano, Kaptagat na Bukar.Serikali, Novemba 2021, ililegeza marufuku hayo kwa kuruhusu kuvunwa kwa miti iliyokomaa katika kipande cha ardhi kisichozidi hekta 5,000.

“Shughuli hiyo itafanywa chini ya usimamizi wa idara mbalimbali za serikali kwa uwazi,” alisema waziri wa Mazingira Keriako Tobiko.

Marufuku hiyo ya serikali imelemaza shughuli katika baadhi ya viwanda vinavyotegemea bidhaa za magogo.

Bei ya gesi nchini imepanda kufuatia mapigano yanayoendelea nchini Ukraine.

Kampuni ya Rubis Energy Kenya ilianza kutekeleza bei mpya ya gesi Jumatatu ambapo bei ya gesi ya kilo sita ilipanda hadi Sh1,560 kutoka bei ya zamani ya Sh1,400.

Kampuni hiyo sasa inajaza mtungi wa kilo 13 kwa Sh 3,340 kutoka Sh2,800.

Mnamo 2021, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) ilianzisha ushuru wa zaida ya thamani (VAT) ya asilimia 16 kwa gesi ya kupikia.

Kutokana na hatua hiyo, bei ya gesi ya kupikia ilipanda kwa Sh300 katika nyingi za kampuni kuanzia Julai 2021 wakati ambapo ushuru huo ulianza kutekelezwa.

Serikali ilianza kutoza ushuru huo wa VAT kwa bidhaa hiyo licha ya malalamishi kutoka kwa Wakenya wengi, haswa wale wa mapato ya chini ambayo maisha yao yalivurugwa na janga la Covid-19.

Awali, Wakenya walifurahia bei nafuu ya gesi kwa sababu serikali haikuwa ikitoza ushuru wa VAT kwa bidhaa hiyo.Ongezeko la hivi punde la bei ya gesi inajiri wakati ambapo vita vinaendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Vita hivyo, vimechangia kupanda kwa bei ya mafuta kote ulimwenguni ikizingatiwa kuwa Urusi ni taifa ulimwenguni linalozalisha mafuta kwa wingi.

Aidha, Urusi ndilo taifa nambari mbili katika uzalishaji wa gesi ya kiasili (natural gas) ulimwenguni.

Bei ya mafuta ghafi inatarajiwa kupanda hadi kufikia dola 150 (Sh15,000) kwa pipa kutoka dola 94 (Sh9,400). Hii ni kwa sababu mzozo wa Urusi na Ukraine umeathiri usafirishaji wa mafuta kutoka Urusi hadi masoko ya nje.

You can share this post!

Kenya Kwanza wataka Timamy awanie ugavana

Mbio za vigari za Karting yavutia madereva 8 wapya

T L