Michezo

Ni mapambano ya piga nyofoa kombe la Europa Liverpool wakisaka muujiza

April 18th, 2024 1 min read

PAMBANO kubwa linasubiriwa ugani Olympic Stadium jijini hapa Alhamisi usiku AS Roma itakapoalika AC Milan katika mkondo wa pili wa robo-fainali ya UEFA Europa League.

Chini ya aliyekuwa ya jagina wa klabu hiyo, Daniele De Rossi aliyeteuliwa mwezi Januari kuwa kocha mkuu, AS Roma imeimarika kwa kiasi kikubwa huku ikiandikisha matokeo ya kuridhisha katika mechi kubwa.

Licha ya kuwa katika nafasi ya tano kwenye ligi kuu ya Italia kufikia sasa baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 55, Roma imekuwa na msururu mzuri msimu huu, huku ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zilizobakia.

Kampeni yake katika michuano hii ya Europa imewezeshwa na mipango kabambe pamoja na kujitolea kwa wachezaji. Kujitolea kwa wachezaji hao kulidhihirika walipoondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Milan ugenini katika mkondo wa kwanza.

Kwa upande mwingine, AC Milan wamekuwa na matokeo mseto, huku washambuliaji wake wakilaumiwa kwa kushindwa kufunga mabao, hasa katika mechi za Serie A, ambako wanashikilia nafasi ya pili kwa pointi 69, nyuma ya Inter Milan.

Kwingineko, baada ya kucharazwa 3-0 nyumbani ugani Anfield, Liverpool watakuwa ugenini Gewiss Stadium mjini Gergamo kujaribu kubadilisha matokeo hayo ya mkondo wa kwanza.

Ratiba ya mechi za Europa League leo:

AS Roma vs AC Milan, Marseille vs Benfica, West Ham United vs Bayer 04 Leverskusen, Atalanta v Liverpool.