Michezo

Ni mguu niponye mchujo wa Qatar ukianza rasmi

September 12th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUWEPO kwa mabingwa wa zamani wa dunia, olimpiki na Diamond League kunatarajiwa kufanya mchujo wa kitaifa wa leo Alhamisi na kesho Ijumaa kwa minajili ya kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar kuwa wa kusisimua zaidi.

Awali, mchujo huu ulitazamiwa kuandaliwa jijini Nairobi kati ya Agosti 20-22 kabla ya Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kuuratibu upya ili kupisha kampeni za Diamond League zilizokamilika jijini Monaco, Ufaransa wikendi iliyopita.

AK inatazamiwa kutumia mchujo wa siku mbili zijazo kuteua jumla ya wanariadha 70 watakaopeperusha bendera ya Kenya jijini Doha kati ya Septemba 27 na Oktoba 6, 2019.

Ingawa hivyo, Elijah Manangoi ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 hatakuwa sehemu ya mchujo huo baada ya kupata jeraha mazoezini. Ni matarajio ya AK kwamba mtimkaji huyo atakuwa amepona kufikia wakati wa kikosi kuelekea Qatar.

Kukosekana kwa Manangoi kutamsaza Timothy Cheruiyot na ulazima wa kuweka hai matumaini ya Kenya katika mbio za mita 1,500 ambazo amezitawala kwa mwaka wa tatu mfululizo kwenye Diamond League.

Wengine watakaowania tiketi ya kuwakilisha Kenya kwenye fani hii ni Charles Simotwo, bingwa wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 (U-20) George Manangoi na Kumari Taki aliyeibuka bingwa wa dunia kwa chipukizi wa U-20 mnamo 2015.

Wanariadha watakaowakilisha Kenya katika marathon kwa upande wa wanaume na wanawake wanatarajiwa kuelekea Doha mnamo Septemba 24 kabla ya kikosi kingine kufunga safari siku moja baadaye.

Vikosi vya Kenya kwa minajili ya marathon na mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanaume na wanawake tayari vimeteuliwa.

Mbali na wanariadha watakaoibuka kwenye nafasi tatu za kwanza katika kila fani mchujoni, mabingwa watetezi wa Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017 pia watapata tiketi za kuwakilisha Kenya jijini Doha.

Wengine watakaofuzu ni wanariadha wote waliohifadhi ubingwa wao katika kampeni za Diamond League msimu huu. Manangoi (mita 1,500), Hellen Obiri (mita 5,000), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka maji na viunzi) na Faith Chepngetich Kipyegon (mita 1,500) ndio wanariadha watakaolenga kuhifadhi mataji waliyoyatwaa 2017.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi kwa upande wa wanawake, Beatrice Chepkoech Sitonik (dakika 8:44.32) alijikatia tiketi tayari baada ya kuibuka mshindi wa taji la Diamond League jijini Zurich, Uswisi mwishoni mwa Agosti 2019.

Ushindani mkali zaidi unatazamiwa katika mbio za mita 800 kwa upande wa wanawake ambapo bingwa wa zamani wa dunia, Eunice Sum atatoana kijasho na Eglay Nalianya, Emily Tuwei, Sylvia Chesebe na Jackiline Wambui ambaye ni malkia wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18.

Kenya imekabiliwa na kibarua kigumu zaidi katika mbio hizi msimu huu kwa upande wa wanaume hasa ikizingatiwa kwamba hakuna mwanariadha yeyote kati ya Ferguson Rotich, Michael Saruni, Cornelius Tuwei na Alfred Kipketer waliowahi kusajili muda wa chini ya dakika mbili katika duru zote za Diamond League.

Bingwa mara mbili wa dunia kwa chipukizi wa U-20 katika mbio za kuruka maji na viunzi, Celliphine Chespol watapigana kumbo na Mercy Chepkurui, Mercy Wanjiru, bingwa wa Afrika Norah Jeruto na mshindi wa nishani ya fedha katika Olimpiki, Hyvin Kiyeng kuwania tiketi mbili zaidi katika fani hii.

Benjamin Kigen, Abraham Kibiwott na Leonard Bett watapigania tiketi tatu nyinginezo katika mbio za mita 3,000 za kuruka maji na viunzi kwa upande wa wanaume.

Watatu watakaotawala fani hii watatoana jasho na Conseslus Kipruto kwa matumaini ya kushindia Kenya nishani zote tatu nchini Qatar.

Margaret Chelimo, Eva Cherono, bingwa mpya wa Afrika Lilian Kasait na malkia wa dunia kwa chipukizi wa U-20, Beatrice Chebet katika ulazima wa kupigania tiketi tatu nyinginezo ili kuungana na Obiri katika mbio za mita 10,000.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa chipukizi wa U-20, Edward Zakayo, Nicholas Kimeli, Richard Kimunyan, Stanley Waithaka na mshindi wa medali ya shaba katika Olimpiki, Paul Tanui watawania tiketi tatu za kuwakilisha Kenya jijini Doha kwenye fainali za mita 5,000 kwa upande wa wanaume.

Millicent Ndoro, Eunice Kadogo, Maureen Thomas na Joan Cherono watapigania tiketi katika mbio za mita 200 kwa upande wa wanawake huku Peter Mwai, Mike Mokamba na Dan Kiviasi wakionyeshana kivumbi kwa upande wa wanaume.