Habari Mseto

Ni miezi kadha gerezani kwa kupiga chafya kiholela jijini

September 28th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

UKITEMBEA katika barabara za Nairobi bila kuwa na kitambaa cha mkono, unajiweka katika hatari ya kutozwa faini ya Sh2000 au kufungwa jela miezi mitatu.

Hii ni kwa sababu sheria inasema mtu anafaa kufunika mapua na mdomo wake kwa kitambaa au karatasi shashi anapopiga chafya.

Ni hatia pia kusubiri magari ya abiria bila kupiga foleni, kutema mate barabarani na kuchuuza bidhaa bila kuwa na beji ya kujitambulisha.

Hizi ni baadhi ya sheria za serikali ya kaunti ambazo zimekuwa zikipuuza na ambazo zinaweza kutia mtu mashakani.

Kuna sheria tano zilizopendekezwa na 18 zilizopitishwa ambazo wakazi wengi wa Nairobi hawazifahamu kama vile kupiga kelele ya aina yoyote barabarani.

Adhabu ya kosa hili ni kutozwa faini ya Sh2000 au kufungwa jela miezi mitatu. Kwa sababu ya kutotekelezwa kwa sheria, barabara za Nairobi zimejaa kelele za kila aina wachuuzi wakitangaza bidhaa zao, makanga wakiita abiria, wahubiri wakipaza sauti na madereva wa matatu wakipiga honi kiholela.

Wamiliki wa majengo wanapaswa kuhakikisha yamepakwa rangi kila mwaka, kudumisha usafi sehemu ya mbele na kuweka taa, jambo ambalo ni ndoto jijini.

Wachache watimiza agizo

Mwaka 2019 Gavana Mike Sonko aliagiza majengo yote jijini – katika kitovu cha jiji – kupakwa rangi lakini ni watu wachache waliotimiza agizo hilo.

Kulingana na sheria za serikali ya kaunti ya Nairobi, ni makosa kuongoza dereva kuingia au kutoka anakoegesha gari. Sheria hii huwa inavunjwa kila siku na watu mbele ya wafanyakazi wa serikali ya kaunti na watu wasiofahamu kwamba, ni hatia kufanya hivyo.

Makosa mengine yanayopuuzwa au ambayo watu hawafahamu ni kuvuta au kusukuma begi kwenye lami na kuendesha mkokoteni, kukata mti bila idhini na kufuga mbwa mwenye umri wa zaidi ya miezi mimne bila kibali.

Mbwa ambao mtu hafai kupata leseni ni wale wa polisi au wanaotumiwa kuongoza watu wenye matatizo ya kuona.