Makala

Ni Mola tu alitukomboa, majeruhi wa Al Shabaab wasimulia

December 10th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MAJERUHI watatu walioponea shambulizi la kilipuzi cha kutegwa ardhini linaloaminika kutekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab eneo la Sankuri, Kaunti ya Lamu Jumamosi, wanasema ni Mungu pekee aliyewaokoa na kuponea kifo kilichokuwa kimewakodolea macho.

Bw Aden Farah, Isse Abubakar na Ahmed Khalif, walikuwa wakisafirisha bidhaa kwa lori lao  kutoka eneo la Hindi kuelekea Kiunga wakati shambulizi hilo lilipotekelezwa majira ya saa tatu asubuhi.

Wakizungumza katika hospitali ya King Fahad mjini Lamu ambako walikimbizwa kwa matibabu, watatu hao walisema hawaamini macho yao kwamba wako hai.

Dereva wa lori lililolipuliwa kwa kilipuzi Aden Farah akieleza masaibu waliyokumbana nayo kwenye shambulizi la kigaidi. Hapa ni hospitalini King Fahad mjini Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Farah ambaye ndiye dereva mkuu wa lori hilo anasema walikuwa wamesafiri kwa takriban masaa mawili unusu kabla ya kusikia mlipuko mkubwa uliopelekea eneo la mbele la gari lao kubomolewa na wao kutupwa nje kwa kishindo kikuu.

Bw Farah alijeruhiwa kwenye paja la mguu wake wa kushoto ilhali wenzake wakiumia zaidi kwenye shambulizi hilo la kilipuzi.

“Yalikuwa malori mawili ambayo yalikuwa yamebeba bidhaa mbalimbali tukielekea Kiunga. Lori langu lilikuwa limetangulia. Tulipopita Mararani tukielekea Sankuri na kisha baadaye Kiunga, ghafla tulisikia mlipuko mkubwa na kilichojiri baadaye ni eneo la mbele la gari letu ambalo lilibomoka na sote watatu tukatupwa nje kwa kishindo kikubwa.”

“Niliumia kwenye mguu. Nilipotazama wenzangu nilishtuka kwani mmoja, Bw Ahmed Khalif ambaye ni utingo wetu alikuwa akivuja damu kila mahali. Haikuchukua muda ambapo wenzetu waliokuwa nyuma yetu waliwasili kwa gari lao na kutuchukua kutukimbiza kwenye zahanati ya Kiunga.”

Bw Ahmed Khalif alipata majeraha mabaya mwilini. Picha/ Kalume Kazungu

“Haikupita muda mrefu tulikutana na maafisa wa usalama ambao walitubeba kwa gari lao na kutukimbiza kwenye zahanati hiyo ya Kiunga na kisha baadaye kutusafirisha kwa ndege hadi kwenye hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu. Kusema kweli ni Mungu tu ndiye aliyetuokoa kwenye tukio hilo la kufisha,” akasema Bw Farah.

Bw Isse Abubakar naye hakuficha machozi ya furaha kwa kuponea chupuchupu kwenye shambulizi hilo la kilipuzi.

Bw Abubakar alimshukuru Mungu na pia walinda usalama waliofanya juhudi kuwakimbiza hospitalini.

“Mungu ndiye aliyetuokoa. Pongezi pia kwa walinda usalama wetu na wote waliofanya juhudi kutufikisha hapa. Japo nimeumia lakini ninafuraha kwamba niko hai,” akasema Bw Abubakar.

Bw Ahmed Khalif aliyejeruhiwa vibaya wakati wa shambulizi hilo akihudumiwa na madaktari na wauguzi hospitalini King Fahad. Atalazimika kusafirishwa mjini Mombasa kwa matibabu maalum. Picha/ Kalume Kazungu

Wakati Taifa Leo ilipozuru kwenye hospitali ya King Fahad, Bw Ahmed Khalif hangeweza kuongea kwani alikuwa hali mahututi na akishughulikiwa na madaktari na wauguzi.

Mmoja wa madaktari aliyezungumza na Taifa Leo Dijitali hospitalini humo alisema mipango tayari ilikuwa inaendelea kumsafirisha Bw Khalif hadi hospitali kuu ya Mombasa kwa matibabu maalum.

“Aliumia vibaya eneo la kifua, tumbo, mgongo, kiuno na miguu. Atalazimika kusafirishwa Mombasa kwa matibabu maalum,” akasema daktari huyo aliyedinda kutaja jina.

Wakati huo huo, usalama umeimarishwa eneo la Sankuri na viungani mwake kufuatia shambulizi la Al-Shabaab lililopelekea watu watatu kujeruhiwa Jumamosi asubuhi.

Afisa Msimamizi wa Operesheni ya Linda Boni, Joseph Kanyiri, alisema msako mkali dhidi ya waliotekeleza shambulizi hilo tayari unaendelea ndani ya msitu wa Boni na vijiji vilivyokaribiana.

“Msako tayari unaendelea dhidi ya waliotekeleza shambulizi hilo. Yeyote mwenye ufahamu kuwahusu wahalifu hao pia atujulishe. Watatu walioumizwa tayari wamekimbizwa hospitalini na maafisa wetu wa usalama,” akasema Bw Kanyiri.