Makala

'Ni muhimu shule nchini Kenya ziwe pahala salama'

September 24th, 2019 4 min read

Na MARY WANGARl na SAMMY WAWERU

MWAKILISHI wa Wanawake wa Kaunti ya Nairobi katika Bunge la Kitaifa, Esther Passaris ameghasika na kituo mojawapo cha runinga nchini kwa kumtaja kama ‘mtu mashuhuri wa majanga’, kuhusiana na mkasa katika shule ya Precious Talents ambapo wanafunzi si chini ya saba walifariki na 64 kujeruhiwa.

Passaris alijitosa kwenye ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo alitofautiana na kituo hicho na kusimulia jinsi alivyochangia kutoa msaada kufuatia kuporomoka kwa darasa katika shule hiyo eneo la Ng’andu Dagoreti Kusini.

“Hakika? Nilikuwa hapo, nikatathmini hali, nikaandaa vinywaji, soda, mkate na maziwa. Nikashukuru waendeshaji bodaboda na vijana wa Ng’ando kwa juhudi zao za kishujaa kabla ya makundi a kukabiliana na dharura kufika. Kisha nikaendelea na shughuli zangu nilizopanga na kuishia KNH saa moja jioni….” alieleza hisia zake.

Mwanasiasa huyo alieleza jinsi alivyotoka baada ya kufahamu kuhusu mkasa huo licha ya kwamba alikuwa mapumzikoni baada ya kufanyiwa upasuaji wiki iliyopita.

“Nitapumzika baadaye mwishoni mwa juma. Singekaa nyumbani. Nilirejesha mgongo wangu “uliopinda” kazini. Hapa ndipo uongozi unapokuwa kujitolea mhanga kwa waliokuweka ofisini wanapokuhitaji. Leo ilikuwa siku ngumu kihisia na kimwili,” alisema.

Hata hivyo, Passaris alisisitiza nia yake ya kuendelea kuhudumia mahitaji ya familia zilizoathiriwa pamoja na wakazi wa eneo hilo kwa jumla.

“Kuhusu suala la watu mashuhuri wa majanga naam. Kuhusu kuhudumia mahitaji ya familia zilizopoteza watoto wao, wanafunzi walio ndani na nje ya hospitali, wazazi wao, walimu na raia wa Wadi ya Ngando, Nairobi, kazi inaendelea kwa kila pumzi kutoka kitandani change hospitalini,” alisisitiza.

Kandi na Passaris, wanasiasa wengine waliofika kwneye eneo la mkasa ambapo darasa liliporomoka ni pamoja na Mbunge wa Dagoreti Kusini, John Kiarie na Seneta aliyeteuliwa Milicent Omanga.

Kituo hicho cha habari kilikuwa kikirejelea viongozi mashuhuri wanaotumia majanga kupata umaarufu kutoka vyombo vya habari na kuwataja kama ‘watu mashuhuri wa majanga.”

“Watu Mashuhuri wa Majanga: Jinsi wanasiasa, viongozi wakuu wanavyojinufaisha kutokana na majanga. Kiarie: Eneo hili halina shule za umma kutokana na unyakuzi wa ardhi. Omanga: Tunalaumu serikali kwa kutotunza shule. Passaris: Wakati wa kampeni tuliahidi kujenga shule hapa..”

Wingu la simanzi liligubika taifa mnamo Jumatatu kufuatia ripoti zilizotikisa taifa kufuatia kuporomoka kwa darasa katika shule ya msingi ya Precious Talent Academy, Barabara ya Ngong, ambapo wanafunzi wanane kati ya umri wa miaka minane na 15 walifariki.

Wanafunzi hao wa Talent Academy, iliyoko eneo la Ng’ando, Dagorretti, walikumbana na mauti mwendo wa asubuhi wakati wakiendelea kudurusu vitabu.

Majeruhi waliripotiwa kuwa 64, ambapo walitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Kenyatta, KNH. Wanafunzi 60 waliruhusiwa kuondoka hospitalini, wanne waliopata majeraha mabaya wakiendelea kupokea matibabu.

Duru zinaarifu madarasa yaliyoporomoka ni ya wanafunzi wa chekechea, lakini walioathirika zaidi ni wa kati ya darasa la 6 hadi 8 ambao walikuwa chini ya ghorofa ya kwanza.

Kuporomoka

Kulingana na walioshuhudia mkasa, jengo hilo liliporomoka dakika kadha kabla ya saa moja asubuhi.

Ni tukio lililoibua maswali chungu nzima hususan kutilia shaka uhalisia wa majengo ya shule za kibinafsi na usalama wa wanafunzi shuleni.

Katika mkasa wa Talent Academy, maafisa kutoka kitengo cha kuangazia majanga ya kitaifa, NDMU, wanadaiwa kufika saa moja baada ya tukio.

Video za runinga zilizopeperesha shughuli za uokoaji moja kwa moja, zilionesha vikosi vya Shirika la Msalaba Mwekundu, St John Ambulance, wafanyakazi wa shule, wakazi na wasamaria wema wakiinua mawe, miti, mbao na mabati kuokoa watoto waliokwama kwenye majengo.

Aidha, walionekana wakitumia mikono na vijiti kuondoa mawe, jambo lililoibua maswali kuhusu kutepetea kujitayarisha kwa kitengo cha majanga ya kitaifa hasa katika kaunti ya Nairobi, kuokoa manusura mikasa inapoibuka.

Mmiliki wa shule hiyo Moses Wainaina alitaja mkasa huo kama ajali ingawa alilaumu halmashauri ya jiji la Nairobi.

Alisema serikali ya kaunti ya Nairobi ilichimba mtaro wa kusafirisha majitaka nyuma ya jengo lililoporomoka, akieleza kwamba hatua hiyo ilifanya madarasa kuwa dhaifu. “Walikuwa na nia njema lakini ajali imetendeka,” akasema Bw Wainaina.

Kuporomoka kwa madarasa ya Talent Academy pia kunaibua maswali kuhusu udhabiti wa majengo jijini Nairobi. Kulingana na halmashauri ya kitaifa ya ujenzi, NCA, kuna zaidi ya majumba 4, 000 Nairobi yanayotakiwa kubomolewa kwa kutoafikia vigezo vifaavyo.

Maeneo yanayotajwa kuathirika zaidi ni Huruma, Kayole, Kariobangi, Zimmerman na mitaa kadhaa Nairobi.

Suala la majengo kuporomoka hususan Nairobi si geni. Mikasa ya aina hiyo hutokea na maafa kufanyika.

Mwaka 2018, jumba la orofa tano eneo la Huruma liliripotiwa kupomoroka na kusababisha vifo vya watu watatu. Mwaka 2017, jengo jingine la ghorofa saba eneo la Embakasi pia liliporomoka.

Katika visa vingi vya aina hiyo, serikali huonekana kutoa mapendekezo mengi na hata maonyo wakati wa tukio, ambayo mwishowe huishia kuwa ahadi hewa.

Viongozi hasa wa kisiasa hutumia jukwaa hilo kujipigia debe na umaarufu kama ilivyoshuhudiwa katika tukio la jana shule ya Talent Academy ambapo mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie, mbunge mwakilishi wa kaunti ya Nairobi Esther Passaris na seneta maalum Millicent Omanga walijijitokeza na kukosoa serikali.

Ni muhimu kukumbusha viongozi hao kuwa wao ndio walioko serikalini kwa sasa na mapendekezo wanayotokoa hasara inapotokea ni sawa na kejeli. Viongozi haohao ndio wenye mamlaka kuunda sheria zitakazoangazia majanga ya aina hiyo katika siku za usoni.

Baadhi ya Wakenya wanawakosoa wakidai wanamwaga machozi ya mamba. Wanashangaa walikokuwa ilhali wakazi walilalamikia udhaifu wa jengo la Talent Academy.

Mtaalamu wa masuala ya ujenzi Lawrence Kariuki, anasema kuna vigezo kadha wa kadha vinavyosababisha majengo kuporomoka.

Kwanza, Bw Kariuki anataja msingi dhaifu na duni katika shughuli za ujenzi, ikiwa ni pamoja na malighafi; vifaa kama vile sarufi, mawe, nyaya, na mbao.

“Madarasa ya Talent Academy yaliyoporomoka ilionekana wazi yalijengwa kwa miti na saruji kukorogewa kwenye nyaya duni. Kwa jumla msingi wake ulikuwa duni na ndio maana yakayumbishwa na majitaka,” anasema, akinyooshea kidole cha lawama wakandarasi walioidhinisha ujenzi wake.

Mtaalamu huyo pia anasema mpango bora wa ujenzi ni miongoni mwa masuala muhimu kuzingatia. Unajumuisha mahali panapolengwa kujengwa pamoja na mafundi wenye tajiriba. Anaeleza kuwa mafundi ambao hawajahitimu ni kichangio cha maporomoko.

Isitoshe, idara za serikali zimegubikwa na ufisadi na majengo duni yanayotakiwa kubomolewa yaliidhinishwa na wadau husika.

Bw Kariuki anasema tamaa na ubinafsi umechangia kuwepo kwa majumba ambayo hayajaafikia vigezo faafu.

“Masaibu tunayoshuhudia ya majengo kuporomoka na kusababisha maafa yanasababishwa na ufisadi katika idara zinazoidhinisha ujenzi. Chanzo cha suluhu ni katika afisi hizohizo zinazotoa idhini,” anapendekeza.