Michezo

Ni mwenye nguvu nipishe The Eagles wakiwania 3-bora

July 16th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

JUMATANO, Julai 17, 2019, itakuwa ni zamu ya Super Eagles ya Nigeria na Carthage Eagles ya Tunisia kupigania medali ya shaba baada ya kupoteza mechi za nusu-fainali Jumapili dhidi ya Algeria na Senegal mtawalia kwenye Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.

Nigeria ya kocha Gernot Rohr ilichapwa 2-1 na Desert Foxes kupitia mabao ya William Paul Troost-Ekong aliyejifunga dakika ya 40 na nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez dakika ya tano ya majeruhi. Odion Ighalo alikuwa amesawazishia Nigeria 1-1 kupitia penalti dakika ya 72 kabla ya Mahrez kufuma frikiki safi dakika ya 95.

Ighalo anaongoza ufungaji wa mabao katika makala haya ya 32.

Baada ya mechi, Rohr alinukuliwa na vyombo vya habari nchini Misri akikubali kushindwa kwa kusema Algeria ilistahili ushindi huo.

Hata hivyo, alikiri kuwa wachezaji wake walilegea katika dakika hizo za majeruhi pengine wakitafuta mechi hiyo iingie muda wa ziada wa daklika 30 katika uwanja wa kimataifa wa Cairo.

“Lilikuwa pigano kubwa hadi dakika ya mwisho. Ilikuwa mechi nzuri. Nadhani wachezaji wangu walitaka mechi iende katika muda za ziada wakidhani kuwa Algeria ilikuwa imechoka zaidi,” kocha huyo Mjerumani alinukuliwa akisema.

Mwenzake kutoka Algeria, Djamel Belmadi alisifu vijana wake kwa “kuonyesha ari kubwa na nguvu za kiakili.”

Tunisia pia ilijifunga bao ikibanduliwa nje ya mashindano haya ya mataifa 24.

Beki Dylan Bronn alicheka na nyavu za timu yake ya Tunisia dakika ya 100 uwanjani 30 June jijini Cairo katika nusu-fainali ya kwanza Jumapili.

Bao hili lilitosha kupatia Teranga Lions tiketi ya kuingia fainali kumenyana na Desert Foxes ya Algeria hapo Julai 19.

Katika mechi ya kutafuta nambari tatu itakayochezewa uwanjani Al Salam jijini Cairo, mabingwa wa Afrika mwaka 1980, 1994 na 2013 Nigeria na asilimia 29 ya kushinda washindi hawa wa mwaka 2004.

Takwimu

Takwimu za ana kwa ana kati ya mataifa haya zinapatia Tunisia asilimia 35 ya kumwaga Wanigeria.

Nigeria, ambayo inajivunia wachezaji wakali kama Ighalo, Alex Iwobi, Ahmed Musa na wengineo, itakuwa ikitafuta kudumisha rekodi ya kutoshindwa na Tunisia hadi mechi nne. Nigeria ilichapa Tunisia kwa njia ya penalti 6-5 katika robo-fainali ya AFCON mwaka 2006 baada ya kutoka 1-1 katika dakika 120.

Mechi mbili zilizopita zilikamilika 0-0 na 2-2 katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2010. Baadhi ya wachezaji matata kwa upande wa Tunisia ni Wahbi Khazri na Taha Yassine Khenissi, ambao ni washambuliaji. Tunisia na Nigeria zinashikilia nafasi za 25 na 45 katika viwango bora vya soka duniani vya FIFA.