Michezo

Ni pata potea kwa Neymar Real na Barcelona zikimtafuta kwa fujo

August 14th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

TETESI kuhusu uwezekano wa Neymar kurejea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona zimeshika kasi kwa mara nyingine baada ya mawakili wa nyota huyu wa PSG, akiwemo Juan de Dios Crespo, kuonekana uwanjani Camp Nou.

Kwa mujibu wa runinga ya Gol TV iliyofichua picha za mawakala hao wa Neymar katika ofisi za Barcelona mnamo Jumatatu, huenda hali iliyotawala mechi ya kwanza ya PSG katika Ligi Kuu ya Ufaransa wikendi jana ikachochea zaidi kubanduka kwa Neymar ugani Parc des Princes.

Wakati wa mchuano huo uliowashuhudia PSG wakiwakung’uta Nimes 3-0, mashabiki walimzomea Neymar peupe huku baadhi wakianika mabango yenye jumbe za kumtaka fowadi huyu wa Brazil kuondoka jijini Paris.

Awali, Barcelona walikariri kwamba hawana uwezo wa kumsajili Neymar msimu huu, kauli iliyomfanya Rais Florentino Perez wa Real Madrid kufichua ukubwa wa kiu ya kujinasia huduma za sogora huyu.

Ingawa hivyo, kocha Zinedine Zidane alionekana kukinzana na bosi wake hasa ikizingatiwa kwamba kubwa zaidi katika azma yake ni kumshawishi kiungo Paul Pogba kuagana na Man-United na kutua ugani Santiago Bernabeu badala ya Neymar kuingia katika sajili rasmi ya Real.

Ilivyo, macho yote kwa sasa yanaelekezwa kwa Neymar ambaye amekabiliwa na panda-shuka tele muhula huu tangu atuhumiwe kumbaka mwanamitindo mzawa wa Brazil na pia kukosa fainali za Copa America kutokana na jeraha.

Kwa upande wao, Real wamesisitiza kwamba watakuwa radhi kujiondoa katika mbio za kumsajili Pogba iwapo Neymar, 27, PSG watakubali kumwachilia kwa ofa ya Sh13 bilioni.

Ili kuwashawishi PSG zaidi, Real ambao watakuwa wakimpokeza Neymar mshahara wa hadi Sh91 milioni kwa wiki, pia wako radhi kuwaachilia Isco, Marcelo na Raphael Varane kutua ugani Parc des Princes ndipo wajipe huduma za Neymar.

Tamanio la Pogba

Ingawa tamanio kubwa zaidi la Pogba ni kuingia Real badala ya kurejea Juventus wanaomwinda usiku na mchana, huenda ikawa vigumu kwa klabu hiyo kufanikisha uhamisho huo hasa baada ya kutumia zaidi ya Sh15 bilioni kujitwalia maarifa ya kiungo Eden Hazard kutoka Chelsea muhula huu.

Kwa mujibu wa Jordi Cardoner ambaye ni Naibu Rais wa Barcelona, njia ya pekee kwa Neymar kurejea Camp Nou kwa Sh26 bilioni zilizotumiwa na PSG kumsajili miaka miwili iliyopita, ni kuongeza wachezaji Ousmane Dembele na Philippe Coutinho juu ya fedha walizonazo kwa sasa.