Habari

Ni Raila Atwoli anayetaka

January 2nd, 2020 2 min read

Na BENSON AMADALA

BAADHI ya viongozi kutoka eneo la Magharibi wamemkashifu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi (Cotu), Bw Francis Atwoli kuwa na njama ya ‘kuiuza jamii kwa Raila’.

Viongozi hao wanasema mpango wa Bw Atwoli kuitisha mkutano baadaye mwezi huu Januari ili kujadili hatima ya Jamii ya ‘Mulembe’ kabla ya uchaguzi wa urais 2022’ una njama fiche.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na wabunge Bernard Shinali (Ikolomani) na Askofu Titus Khamala (Lurambi) walidai Bw Atwoli mwenyewe ‘ni mgeni’ kwa kuwa haishi eneo la Magharibi, na kwa hivyo hana mamlaka ya kulazimishia eneo hilo mtu wa kumpigia kura za urais.

Bw Atwoli amenukuliwa akisema mkutano utakaofanywa katika uwanja wa Bukhungu Januari 18, utakuwa wa kumteua Msemaji wa jamii hiyo, atakayeiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Kinara huyo wa Cotu alitamka hayo nyumbani kwake Khwisero Alhamisi wiki iliyopita baada ya kufanya mkutano na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo walikuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Mwakilishi wa kinana mama kaunti ya Kakamega Elsie Muhanda, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Mbunge Maalum Wilson Sossion.

Lakini Bw Wetang’ula na wenzake walisema jamii hiyo haitapumbazwa kumuunga mkono mwaniaji kiti cha urais kutoka eneo lingine.

“Tunajua ajenda yao na hatutakubali watu kutoka nje wasambaratishe juhudi zetu za kuunganisha Jamii ya Waluhya kutetea eneo lao,” alisema Bw Wetang’ula.

Askofu Khamala alisema Waluhya hawatakubali “kutawalwa na watu kutoka nje” kuhusu watakaye muunga katika kinyang’anyiro cha Urais 2022. Viongozi wote wa jamii ya Waluhya watakutana Nairobi kuamua mwelekeo wao kisiasa. Hatuhitaji kiongozi kutoka nje kutupa mwelekeo,” akasema Askofu Khamala.

Ingawa hawakumtaja Bw Odinga moja kwa moja, viongozi hao wanaamini kuwa ukuruba wa Bw Atwoli na Bw Odinga unamfanya asiwe mpatanishi huru kwa jamii hiyo.

Seneta huyo wa Bungoma alisema kuwa ameshirikiana na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kuhakikisha eneo hilo limempigia kura mwaniaji mmoja wa urais wakati wa uchaguzi mkuu.

Jamii ya Waluhya ambayo imekuwa ya pili kwa idadi kubwa ya wapigakura nchini, imeshindwa kuwa na mwaniaji urais tangu 1997. Hata wakati huo, kulikuwa na Michael Wamalwa Kijana na Martin Shikuku, ambao kwa pamoja walipata jumla ya kura 541,844 pekee kati ya kura 6 milioni zilizopigwa. Nafasi ya karibu zaidi ya kupata mwaniaji ilikuwa 2013, Bw Musalia Mudavadi iliposemekana angeliteuliwa, kabla ya kuchujwa katika kisa kinachotambuliwa zaidi kwa jina la utani ‘madimoni.’

Viongozi hao walisema hayo wakati wa tamasha za kitamaduni za Abatsotso zilizofanyika Ikonyero eneo la uwakilishi bungeni la Lurambi.

Bw Wetang’ula aliwasihi Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kuhakikisha ripoti ya BBI imetekelezwa kwa haraka.

Alisema mikakati ya kisheria inapasa kuwekwa kuhakikisha ripoti hiyo imetekelezwa katika muda wa miezi minne ijayo.

“Hatutaki utekelezaji wa ripoti ya BBI uchukue muda mrefu hadi uchaguzi wa 2022 upite kisha isambaratishwe,” alisema Bw Wetang’ula.