Michezo

Ni rasmi Gor Mahia itawakilisha Kenya katika CAF Champions League

May 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limewasilisha rasmi jina la Gor Mahia kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ili wajumuishwe katika kampeni za kuwania taji la Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) msimu ujao.

Mnamo Alhamisi iliyopita, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF, alitamatisha kampeni za msimu huu mzima wa soka ya humu nchini na kutawaza Gor Mahia mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) 2019-20.

Bidco United walioibuka wa pili katika Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) walijiunga na Nairobi City Stars kupanda ngazi hadi KPL ili kuchukua nafasi za SoNy Sugar na Chemelil Sugar walioteremshwa daraja.

Kisumu All-Stars walioshikilia nafasi ya 16 kwenye jedwali la KPL watachuana na Vihiga United waliomaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu kubaini kikosi cha ziada kitakachoshuka daraja kwenye KPL na kitakachopanda ngazi kutoka NSL kwa minajili ya kinyang’anyiro cha muhula ujao.

Kwa mujibu wa FKF, Mwendwa alitumia ibara ya 2.6.1.2 katika kifungu cha kanuni za shirikisho hilo kutawazwa mshindi na kuamua vikosi vya kushuka ngazi katika ligi zote za soka ya humu nchini msimu huu.

Ingawa hivyo, maamuzi hayo ya FKF yamepingwa vikali na idadi kubwa ya washikadau, ikiwemo klabu ya Kakamega Homeboyz iliyoambulia nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia.

Kati ya wengine waliokashifu hatua ya FKF ni Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL Jack Oguda, mwenyekiti wa zamani wa FKF Sam Nyamweya, mwenyekiti wa Chemelil Moses Adagala na Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Lordvick Aduda.

“Tumewaandikia CAF na sasa ni rasmi kuwa Gor Mahia watapeperusha bendera ya Kenya katika kipute cha CAF Champions League msimu ujao,” akatanguliza Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

“Tumewafafanulia kwamba kwa sababu ya janga la corona, ilitulazimu kutamatisha Ligi Kuu ya KPL na tukaongozwa na kanuni za FKF kutawaza Gor Mahia mabingwa wa kipute hicho msimu huu,” akaongeza.

Gor Mahia watakuwa wakirejea katika ulingo wa soka ya kimataifa barani Afrika kwa msimu wa nne mfululizo na watapania kuboresha matokeo yao ya muhula jana na angalau kutinga hatua ya makundi.

Katika msimu uliopita, Gor Mahia walibanduliwa mapema katika raundi ya kwanza baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 6-1 na USM Alger ya Algeria.

Mnamo Aprili 28, CAF iliwapa FKF makataa ya hadi Mei 5 kuwaarifu kuhusu mustakabali wa msimu huu wa 2019-20 katika vipute vya KPL na FKF Shield Cup.

“Tungependa kufahamu hali ilivyo kwa sasa katika KPL na mashindano mengine ya kuwania ubingwa wa makombe ya kufuzu kwa mechi za CAF. Tufahamisheni mikakati yenu katika juhudi za kutamatisha msimu huu na iwapo mnatarajia kukamilisha mechi zilizosalia au kuzifutilia mbali. Hili litatuwezesha kuweka mipangilio itakayofanikisha kampeni za msimu ujao,” ikasema barua hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa CAF, Abdelmounaim Bah.