Ni rasmi kuwa Martha Koome ndiye Jaji Mkuu wa Kenya

Ni rasmi kuwa Martha Koome ndiye Jaji Mkuu wa Kenya

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amemteua rasmi Martha Koome kuwa Jaji Mkuu wa Kenya kupitia notisi kwenye toleo rasmi la gazeti la serikali.

Kiongozi wa taifa alichukua hatua hiyo muda mfupi baada ya bunge la kitaifa kumwidhinisha Jaji Koome kwa wadhifa huo.

Wabunge walipiga kura kwa kauli moja kuhusiana na ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) iliyompiga msasa Jaji huyo kwa wadhifa huo wiki jana baada ya kupendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Jaji Koome sasa anarithi cheo hicho kutoka kwa David Maraga aliyestaafu mnamo Januari 12, 2021 baada ya kuhudumu kuanzia Januari 12, 2016.

Aidha, Koome mwenye tajriba ya miaka 33 katika taalamu ya uanasheria, anakuwa Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke tangu Kenya ilipopata uhuru 1963.

Ni mtu wa 15 kushikilia wadhifa huo nchini na wa tatu kufanya hivyo chini ya katiba ya sasa; nyuma ya Bw Maraga na Dkt Willy Mutunga.

Jaji Koome amejijengea sifa katika sheria ya familia na hutetea zaidi haki za watoto na akina mama, sifa ambayo ilimsaidia kutuzwa na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2020.

Wakati wa majadala kuhusu ripoti ya JLAC iliyomwidhinisha, Jaji Koome kwa cheo cha Jaji Mkuu, wabunge wanawake walimmiminia sifa wakisema uteuzi wake ni fahari kubwa kwa jinsia ya kike nchini.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alimtaja kama mwanasheria mwenye maono na anayefahamu fika wajibu mkubwa unaomsubiri katika Idara ya Mahakama.

“Ni sawa kwa Kenya kuwa na Jaji Mkuu mwanamke, Naibu Jaji Mkuu mwanamke na wengine wenye hadhi ya juu katika asasi hiyo. Lakini sasa tusitumie ufanisi huo kama kisingizio cha kuwaondoa wanawake kutoka nyadhifa nyingine kuu serikalini,” akaeleza.

Kando na Bi Koome na Jaji Philomena Mwilu ambaye ni Naibu Jaji Mkuu, wanawake wengine wanaoshikilia vyeo vya juu katika Idara ya Mahakama ni Naibu Mwenyekiti wa JSC Profesa Olive Mugenda, kaimu Rais wa Mahakama ya Rufaa Wanjiru Karanja, Kiongozi wa Majaji wa Mahakama Kuu Lydia Achode, Kiongozi wa Majaji wa kitengo cha Mahakama ya Mazingira na Masuala ya Ardhi, Maureen Onyango, Msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi, Msajili wa Mahakama Kuu Judy Omange, Msajili wa Mahakama ya Juu Esther Nyaiyaki na Msajili wa tume ya JSC Frida Mokaya.

You can share this post!

Maafisa wa DCI wakita kambi Kilifi kupeleleza serikali ya...

Kocha Joachim Loew arejesha wanasoka Muller na Hummels...