Michezo

Ni rasmi sasa klabu ya Ayub Timbe ‘yaingia nyasini’ baada ya kusikitisha Ligi Kuu ya China

November 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BEIJING Renhe, ambayo ni klabu iliyoajiri Mkenya Ayub Timbe, imefeli katika juhudi zake za kukwepa kuangukiwa na shoka kwenye Ligi Kuu ya Uchina baada ya kuzabwa 3-2 na Jiangsu Suning katika mechi muhimu Jumamosi.

Renhe, ambayo inavuta mkia katika nafasi ya 16, ilihitaji kushinda mechi zake zote zilizosalia dhidi ya Jiangsu Suning (Novemba 23), Shanghai SIPG (Novemba 27) na Dalian Yifang (Desemba 1) na kuomba nambari 14 Tianjin Tianhai na nambari 15 Shenzhen ziteleze ili iepuke kushushwa, imezamishwa na mabao kutoka kwa Mbrazil Alex Teixeira na raia wa Croatia Ivan Santini aliyetikisa nyavu mara mbili.

Mabao yote ya wapinzani yalipatikana katika kipindi cha kwanza, huku Renhe, ambayo ilikuwa nyumbani, ikijiliwaza na mabao kutoka kwa Mholanzi Elvis Manu na raia wa Senegal, Makhete Diop dakika za 55 na 59, mtawalia. Winga matata Timbe hakushiriki mchuano huu baada ya kupata jeraha la kifundo dhidi ya Misri katika mechi ya kwanza ya Harambee Stars ya Kundi G ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2021 iliyosakatwa mjini Alexandria mnamo Novemba 14.

Renhe, ambayo iliingia mchuano huu bila ushindi dhidi ya Jiangsu Suning, imezoa alama 13 pekee kutokana na mechi 28. Hata ikishinda mechi zake mbili zilizosalia haiwezi kufikia Tianhai na Shenzhen zilizozoa alama 22 na 20, mtawalia.