Ni Ruto au Raila? PAA yajipata ikijikuna kichwa

Ni Ruto au Raila? PAA yajipata ikijikuna kichwa

Na BRIAN OCHARO

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachohusishwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, sasa kimeanzisha mchakato wa kutambua mgombea urais atakayeungwa mkono kati ya wanasiasa ambao tayari wametangaza azimio lao la urais.

Wiki iliyopita, Taifa Leo ilibainisha tofauti zilizopo baina ya wafuasi wa chama hicho ambapo baadhi yao wanataka kiunge mkono Kiongozi wa ODM Raila Odinga huku wengine wakimtaka Naibu Rais William Ruto.Chama hicho tayari kiliamua hakitakuwa na mgombeaji wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Katika mkutano wa wajumbe uliofanywa Mombasa, msemaji wa kikundi cha viongozi wa zamani wa Pwani, Bw Lucas Maitha, alikiri kuwa kwa sasa chama hicho hakijapata nguvu za kutosha kusimamisha mgombeaji wake wa urais mwaka 2022.

Mkutano huo wa Jumatatu ulihudhuriwa na wajumbe kutoka kaunti zote sita za Pwani wakiwemo wabunge wa zamani na watumishi wa umma waliostaafu.

“Lengo letu sio kusimamisha mgombea wa rais kwa sasa kwa sababu tunajua kwamba nafasi ya kiongozi wa PAA kunyakua kiti hicho ni ndogo. Hata hivyo, tuko tayari kufanya kazi na viongozi wengine,” akasema Bw Maitha, ambaye ni mbunge wa zamani wa Malindi.

Alieleza kuwa, wamejitolea kushirikiana na mgombeaji yeyote ambaye atadhihirisha ana uwezo wa kutatua changamoto zinazokumba ukanda huo. Kufikia sasa, wagombeaji wakuu wa urais ambao wameonekana kupeana ushindani mkubwa ni Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto ambao wamefanya kampeni nyingi za uchaguzi ujao Pwani.

“Tutazungumza na kujadiliana na yeyote atakayetaka uungwaji mkono kutoka kwetu. Bw Odinga au Dkt Ruto wakitualika tutawasilisha masuala ambayo tungetaka yashughulikiwe,” akasema Bw Maitha.

Chama hicho hata hivyo kimeshikilia kuwa kitasimamisha wagombea wa viti vilivyosalia.

Bw Kingi alisema kongamano la Jumatatu liliitishwa ili kusaidia katika kupanga mustakabali wa kisiasa wa uchaguzi wa mwaka 2022 na hata baadaye.

“Kila eneo nchi nzima linapanga mustakabali wake wa kisiasa, eneo la Pwani lazima lisisalie nyuma. Eneo hili limeruhusu watu wengine kufanya maamuzi kwa niaba yake lakini safari hii tumesema imetosha. Wakati umefika ambapo eneo hili lazima lipange mwelekeo wake wa kisiasa kabla na baada ya uchaguzi mkuu,” akasema Bw Kingi.

Chama hicho wiki ijayo kinatarajiwa kufanya mashauriano na vyama vingine vya Pwani ili kuunda muungano mmoja utakaoshirikishwa katika siasa za kitaifa.

Majadiliano kuhusu uundaji wa muungano huo wa Pwani kutoka kwa vyama vya Kadu-Asili, Shirikisho, Republican, Umoja Summit na Communist yamekuwa yakikumbwa na changamoto tele.Chama cha Kadu-Asili tayari kiliamua kujiunga na Muungano wa One Kenya Alliance wiki chache zilizopita.

“Tumekubaliana kwamba mara tu tutakapounganisha vyama hivi kuwa chombo kimoja, mazungumzo yoyote yatafanywa kupitia viongozi wa muungano huo wala si na mtu binafsi,” akasema Bw Maitha.

You can share this post!

Uhuru asema Raila na Mudavadi ndio walimjulisha bungeni

Mama mboga ‘aoza’ binti kwa mteja wa kila siku

T L