HabariSiasa

Ni sharti mahakamma ilinde haki za Jaji Mwilu – Kalonzo

August 30th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA makamu wa rais Kalonzo Musyoka Jumatano alimsihi hakimu mkuu Lawrence Mugambi asitishe kusikizwa kwa kesi dhidi ya naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu anayekabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya mamlaka na kupokea mkopo wa Sh12 milioni kutoka kwa benki iliyofilisika ya Imperial.

Bw Musyoka aliomba mahakama izingatie mikataba ya Umoja wa Kimataifa ya kutetea haki za binadamu.

“Kifungu nambari 50(2) cha Katiba kinaamuru haki za kila mshukiwa zilindwe. Kumsomea DCJ Mwilu mashtaka ilhali amewasilisha kesi katika mahakama kuu ya kupinga kushtakiwa kwake ni ukiukaji wa haki zake,” alisema Bw Musyoka.

Alimsihi Bw Mugambi asitishe kesi hiyo hadi mahakama kuu iamue ikiwa kuna kesi iliyo na mashiko ya kisheria au la.

Bw Kimuli anayemtetea wakili  Stanley Kiima alisema ni jambo la kusitikisha sana ikiwa Mkenya atashtakiwa kwa kutenda kazi yake rasmi.

“Bw Kiima alishtakiwa kwa kumwakilisha Jaji Mwilu katika suala la kuomba mkopo katika Benki ya Imperial zaidi ya miaka mitano iliyopita. Alitekeleza jukumu lake kama wakili aliyemwakilisha DCJ. Mbona ashtakiwe sasa?” akauliza Bw Kimuli.