Siku 365 za kufa kupona

Siku 365 za kufa kupona

Na CHARLES WASONGA

NI mwaka wa lala-salama taifa linapokaribisha siku 365 zenye pilkapilka tele za kisiasa huku macho yote yakiwa kwa wagombeaji wa kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Katika kipindi cha miezi 12 ijayo, wanasiasa wanaokimezea mate kiti cha urais wanatarajiwa kuendeleza kasi ya kampeni zao katika mazingira yaliyobanwa na masharti yaliyowekwa na serikali kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo, wagombeaji wakuu, kama vile, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi wamebuni mbinu ya kuendesha kampeni zao kupitia majukwaa ya makanisa na kukutana faraghani na makundi mbalimbali.

Japo, Bw Odinga hajatangaza waziwazi kwamba atawania urais, mwanasiasa huyo mkongwe amekuwa akitangaza sera mbalimbali ambazo ananuia kutekeleza endapo atafanikiwa kuunda serikali ijayo.

Kufikia sasa ametoa ruwaza yake inayojikita katika ukuzaji wa uchumi kuanzia ngazi ya vijiji, uboreshaji wa utumishi wa umma na kufanikisha mabadiliko katika sekta ya afya kupitia utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote (UHC).

Bw Odinga amedokeza atatangaza rasmi azma yake ya urais mwishoni mwa mwezi huu baada ya mahakama ya rufaa kutoa uamuzi kuhusu mswada wa mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

“Mwishoni mwa Agosti, tutatoa tangazo kubwa ambalo litasababisha Tsunami kubwa katika uwanja wa siasa nchini. Hata hivyo, wakati huu tunasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu hatima ya BBI na tuko tayari kukubali uamuzi wowote utakaotolewa kwa sababu mimi na Rais Kenyatta ni wanademokrasia,” akasema Julai kwenye mahojiano na Radio Citizen nyumbani kwake Karen, Nairobi.

Jopo la majaji saba wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Daniel Musinga, hapo Agosti 20 litatoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa mbele yalo na wakereketwa wa BBI kupinga hatua ya mahakama kuu kuharamisha mageuzi hayo ya katiba.

Katika kipindi cha miezi 12 ijayo, Dkt Ruto, ambaye ametangaza azma yake ya kuwania urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) baada ya kugura Jubilee, anatarajiwa kuendeleza kampeni zake licha ya kudinda kugura chama hicho tawala.

“Sisi si wageni popote pale. Tunajiunga na vyama vya kisiasa kwa hiari na kuondoka kwa hiari. Hamna anayepaswa kuuliza kwani tungali hapa. Hatukualikwa nchini,” akasema Alhamisi baada ya kuongoza mkutano wa wabunge wanaoegemea mrengo wa Tangatanga.

Dkt Ruto alikuwa akijibu miito ya wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaomtaka kujiondoa rasmi kutoka Jubilee na serikalini badala ya kuendelea kuikosoa akiwa ndani.

Mkutano huo uliofanyika katika makazi rasmi ya Naibu Rais, mtaani Karen pia ulijadili mikakati ya kuvumisha sera yake mpya ya kuchochea ukuaji wa uchumi kutoka mashinani, kuendelezwa kwa shughuli za usajili wa wanachama wa UDA na kufanyika chaguzi za mashinani za chama hicho kuanzia Oktoba 2021.

Kuanzia sasa hadi mwezi Mei 2022 wakati vyama na miungano, itakapoanza kuteua wagombeaji wa urais, Dkt Ruto na Bw Odinga watakabiliwa na kibarua kigumu cha kuteua wagombeaji wenzao.

Duru zinasema wawili hao wanatarajiwa kuteua wagombeaji wenza kutoka eneo la Mlima Kenya endapo eneo hilo halitatoa mgombeaji urais mwenye ushawishi mkubwa kumzidi Bw Muturi anayetoka eneo la Mlima Kenya mashariki.

Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaoshirikisha Mbw Musyoka, Mudavadi, na kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula watakabiliwa na kibarua cha kuamua ni nani kati yao atakayepeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais.

Mbw Musyoka na Mudavadi wamekuwa waking’ang’ania nafasi hiyo huku kila mmoja akidai ndiye anayefaa kupambana na Dkt Ruto na Bw Odinga katika uchaguzi hui

Mbali na wagombeaji urais, macho ya Wakenya yataelekezwa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo inakabiliwa na kibarua kizito cha kufanikisha maandalizi ya uchaguzi mkuu huku ikilalamikia bajeti finyu. Kulingana na mpango wake kuhusu uchaguzi (Election Operations Plan-EOP) wa hadi Agosti 9, 2022, IEBC imeorodhesha shughuli kadhaa ambazo zitahitaji fedha nyingi.

Kuanzia Septemba, IEBC itaanza kutekeleza mpango huo kwa kuzindua usajili wa wapigakura kwa halaiki.

Tayari tume hiyo imetangaza zabuni ya ununuzi wa vifaa vya kutumika katika uchaguzi mkuu ujao.

Septemba IEBC, inatayariwa kupata makamishna wanne wapya walioteuliwa na Rais Kenyatta wiki hii.

Wao ni; Francis Wanderi, Justus Abonyo, Juliana Cherera, na Irene Cherop ambao majina yao yamewasilishwa bungeni kupigwa msasa.

You can share this post!

Polo aporwa na kisura ‘malaika’

DIMBA: Ruby: Beki mtulivu akiwa na boli na mkali wa...