Habari Mseto

Ni tabia mbaya kuanzisha vyama vya akiba na mikopo kwa lengo la kuwapunja wanachama – Rais Kenyatta

October 23rd, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta amefanya ziara katika eneo la Pumwani, Nairobi, Ijumaa ambapo amechukua fursa kulaani tabia ya baadhi ya watu kuanzisha vyama vya akiba na mikopo kwa lengo la kuwapunja wanachama.

Aidha, kiongozi huyo wa nchi amesema uaminifu ndio nguzo ya ufanisi wa jambo lolote lile linaloanzishwa kwa manufaa ya kuimarisha.

Akikiri kuwa uongozi si jambo rahisi, Rais Kenyatta amesema muhimu zaidi kwa kiongozi ni kukuza uaminifu kwa anaowaongoza.

“Kuwa kiongozi si rahisi. Hakuna kitu kigumu kama kuwa kiongozi na nyakati zingine unahitaji kufanya maamuzi thabiti na yatakayoleta imani kwa unaowaongoza. Kumekuwepo changamoto katika vyama vya akiba na mikopo, ambapo waasisi hushawishi watu kuweka akiba kisha wanavivunja ghafla na kutoweka na pesa zao,” akasema Rais Kenyatta alipokutana na wawakilishi wa wahudumu wa bodaboda nchini katika ukumbi wa mikutano ulioko Pumwani.

Rais aliibua mdahalo huo kufuatia kisa cha hivi karibuni katika matembezi yake Kisii, baada ya kupokea rasmi ripoti iliyoandaliwa na jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI), alichotaja kilizua masuala ya utovu wa uaminifu.

Alisema baada ya kukutana na baadhi ya wahudumu wa bodaboda Kisii, na kujitolea kuwapiga jeki kifedha kama kundi, ukosefu wa imani kwa viongozi ulijitokeza bayana.

“Nilitoa mapendekezo mawili; niwape fedha waweke kama akiba au mtu binafsi na nishushe kiwango nilichonuwia kuwapa kama kundi. La kushangaza, walipendekeza nishushe,” akasimulia kiongozi huyo wa nchi, akionekana kutamaushwa na hatua hiyo iliyoibua maswali ya uaminifu.

Ni kupitia tukio hilo, Rais Kenyatta amehimiza viongozi wa Sacco na pia makundi yaliyoundwa kwa minajili ya kuweka akiba, kuthamini “uaminifu” akisema ndiyo hulka na sifa ya kipekee inayoleta ufanisi na maendeleo.

“Hakikisha unaoongoza wanakuamini. Unavyoshughulikia raslimali zao, ikiwa ni kwa njia ya uaminifu, ndivyo wataweka akiba kwa wingi,” Rais akashauri.

Rais Kenyatta amehimiza haja ya watu kubuni vyama vya ushirika au makundi ili kufanikisha miradi ya maendeleo. “Usipojipanga, utakuwa mtu wa kutumiwa. Unapoanzisha chama cha kuweka akiba, hakikisha wanachama wanaweza kufuatilia fedha zao kwa njia ya simu. Mtu akitaka pesa, si mambo ya kuenda kwa mwenyekiti eti niwekee kidole hapa…hapana, imani iwepo,” akafafanua Rais.

Baadhi ya waanzilishi wa vyama vya ushirika wamejipata pabaya kwa sababu ya kutapeli umma. Serikali haijaweka mikakati wala sheria maalum kuvilainisha na kuhakikisha fedha za wanachama ni salama.