Ni tikiti ya Shahbal, Maitha ugavana wa Mombasa

Ni tikiti ya Shahbal, Maitha ugavana wa Mombasa

NA VALENTINE OBARA

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal, leo Alhamisi anatarajiwa kumtangaza rasmi Bi Selina Maitha Lewa, dadaye mbunge wa zamani wa Kisauni marehemu Karisa Maitha, kuwa mgombea mwenza wake wa ugavana Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Shahbal, ambaye anatumai kutwaa tiketi ya ODM kuwania kiti hicho, amewatangulia wapinzani wake katika hatua hiyo kwa maandalizi ya kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha gavana Hassan Joho.

Kujitosa kwa Bi Lewa katika siasa za urithi wa ugavana Mombasa, kunatarajiwa kufufua mdahalo kuhusu mchango wa marehemu Maitha katika siasa za Pwani.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bi Lewa alisema ingawa ni mara yake ya kwanza kujitosa katika siasa, alikuwa na uhusiano wa karibu sana na kakake na hivyo ana ari ya kuendeleza maazimio ambayo Maitha alitaka kufanikisha.

Maitha alifariki akiwa katika ziara rasmi ya kiserikali nchini Ujerumani mnamo 2004.

“Nimezaliwa katika familia ya wanasiasa lakini mimi mwenyewe sijakuwa mwanasiasa. Kakangu tulikuwa naye guu kwa guu. Kufikia wakati ambapo aliaga dunia, alikuwa amejitolea kutumikia watu wake kikamilifu,” akasema.

Marehemu Maitha aliacha sifa tele za kuwa mmoja wa wanasiasa wakakamavu katika siasa za Pwani, hali iliyomfanya kupewa jina ‘mugogo’ kuashiria ndiye ‘mfalme’ wa Wamijikenda kisiasa.

Malengo

Tangu kufariki kwake, wanasiasa wa Pwani wamekuwa wakijitahidi kupata msemaji ambaye anaweza kufikia hadhi yake lakini juhudi hizo hugonga mwamba kutokana na migawanyiko ya viongozi.

“Ile kazi ambayo kaka (Maitha) aliianzisha, nataka kuimaliza. Alitaka vijana wapate kazi, barabara zijengwe na kadhalika. Malengo yangu ni kuwezesha watu kupata ufadhili wa masomo, vijana wapate kazi kwa njia nyingi wala si kutegemea tu kazi katika serikali ya kaunti. Kuna njia kama vile kufungua viwanda, kutafuta uhusiano mwema na sekta ya biashara za kibinafsi nje na ndani ya nchi ili vijana wapate kazi,” akaeleza.

Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa mgombea mwenza wa Shahbal, Bi Lewa alikuwa Naibu Kamishna wa Kaunti aliyesimamia Kaunti Ndogo ya Machakos, hadi Januari 2022.

Kwa mujibu wa wasifu wake, aliwahi pia kuhudumu kama Naibu Kamishna wa Kaunti, Jomvu, Mombasa mnamo 2019, msaidizi wa kibinafsi wa Kamishna wa Pwani mnamo 2018, na Naibu Kamishna wa Kaunti, Kilifi Kaskazini mnamo 2015.

Aliwahi kuhudumu katika nyadhifa nyingine za utawala Kikambala, Bahari, Malindi zote zilizoko Kaunti ya Kilifi, mbali na Bomet, Narok, Msambweni na Kiambu katika miaka iliyotangulia.

Mbali na kazi zake serikalini, aliwahi kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya serikali.

Alieleza kuwa, ujuzi alioupata katika kazi hizo umemwezesha kuwa mweledi wa masuala ya usimamizi na uongozi wa kijamii.

“Nimekuwa afisa msimamizi kwa muda mrefu. Nimefanya kazi serikalini kwa miaka 18 na katika mashirika ya kijamii miaka miwili. Kwa jumla nina tajriba ya miaka 20 ya kufanya kazi na jamii. Hata nikifanikiwa kuwa naibu gavana bado nitakuwa msimamizi,” akasema.

Kulingana naye, uamuzi wa kujitosa katika siasa za uongozi wa kaunti ulitokea baada ya mashauriano ya kina na Bw Shahbal.

Vile vile, alisema alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia ajenda ya Bw Shahbal kuhusu kuboresha hali ya maisha ya wakazi.

“Azma yangu ni kutumikia watu wa nyumbani. Nilipokuwa serikalini, nilifanya mengi katika kaunti za watu wengine, sasa nataka kutumikia watu wetu. Mimi ni mtumishi wa watu,” akasema.

Bi Lewa alitoa wito kwa wanawake wa Pwani kujitokeza mapema kushiriki katika masuala ya uongozi na siasa iwapo wanaazimia kushikilia nyadhifa za uongozi katika siku za usoni.

Alisema baadhi ya wanasiasa wa kike katika maeneo ya Pwani ambao sasa wanaazimia kuwania ugavana na wanatoa ushindani mkali dhidi ya wapinzani wao, walianza safari yao mapema katika nyadhifa nyinginezo.

“Siasa inataka ukakamavu. Ili mwanamke apate mtoto ni lazima apitie hatua tofauti. Katika kila njia lazima uwe mkakamavu. Lazima uanzie mahali fulani. Kuna hatua ambazo ni lazima upitie. Ukitaka kuota lazima ulale. Mimi nililala nikaota na ndoto yangu lazima itimie,” akasema.

Naye Bw Shahbal alisema kwamba uamuzi wake kumteua Bi Lewa ulitokana na sababu kuwa ameridhishwa na uwezo wake wa utendakazi katika utawala.

Alisema pia kuwa haijalishi Bi Lewa ni limbukeni katika siasa. Kilicho muhimu ni kufahamu shida za wananchi zinazohitaji kutatuliwa.

Alisema suala kuwa Bi Lewa ni mwanamke au ametoka katika familia mashuhuri ya kisiasa ya Maitha halikuwa kigezo katika uteuzi wake.

“Kina mama wanahitaji kujumuishwa katika uongozi, kwa hivyo ni muhimu kuwapa nafasi. Hata hivyo, si jinsia pekee iliyo muhimu. Kilicho muhimu zaidi ni kuangalia uwezo wa mtu. Mahali anakotoka kitaaluma kumempa uwezo wa kuelewa mfumo wa utawala wa serikali. Pia hatukuzingatia sana kwamba ni jamaa ya familia ya kisiasa ya Maitha,” akaeleza Bw Shahbal.

Alisema kuwa wakati mtu anateua mgombea mwenza, ni muhimu kutilia maanani uhalisia kwamba huyo ndiye anayeweza kurithi kiti cha ugavana endapo jambo lolote litamkumba gavana kabla kipindi chake cha uongozi kukamilika.

Matukio yanayoweza kuzua hali hii kikatiba ni ikiwa gavana atatimuliwa mamlakani au akifariki.

Alipuuzilia mbali dhana kuwa ameharakisha kutangaza anayemtaka kuwa mgombea mwenza, akisema ana mpangilio maalumu na mahasimu wake wa kisiasa sasa wana mfano wa kuiga.

You can share this post!

Mwanamuziki Rocky asifiwa

Karua aingia boksi

T L