Ni uchaguzi wa masonko 2022

Ni uchaguzi wa masonko 2022

WINNIE ATIENO na VALENTINE OBARA

MABILIONI ya pesa yataanza kumiminika kitaifa hivi karibuni, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuchapisha viwango vya fedha ambazo wanasiasa watakubaliwa kutumia kuendesha kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na gazeti rasmi la serikali lililochapishwa jana, wanasiasa wanaotaka kuwania viti mbalimbali kuanzia udiwani hadi urais watakuwa huru kutumia mamilioni ya pesa kwenye kampeni zao.

Ingawa IEBC imeweka viwango vya juu vya pesa, bila shaka kuna wale watakaotumia ujanja kuvipitisha kwa kuwa hakuna mfumo mwafaka wa kufuatilia gharama za kampeni za wanasiasa wote.

Haya huenda yakawafungia nje wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha ilhali wana uwezo wa kuwa viongozi wasifika.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati jana alitoa wito kwa wabunge kupitisha sheria zinazohusu matumizi ya fedha za kampeni ili mwongozo waliotoa utekelezwe kikamilifu.

“Tunaomba bunge lipitishe sheria hizo ambazo tuliweza kupeleka mswada wao bungeni 2016, ili tuwe na usimamizi bora kuhusu ufadhili wa kampeni za wanasiasa. Sisi tumechapisha viwango ambavyo vinafaa kutumiwa katika gazeti rasmi la serikali inavyohitajika kisheria. Hiyo itawezesha wadau kutoa mchango wao kama wangependa kuwe na marekebisho,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika kongamano la wadau wa uchaguzi lililoandaliwa na Shirikisho la Wahariri la Kenya (KEG) katika Kaunti ya Mombasa, ambapo alizidi kushinikiza serikali iongezee tume yake pesa ili kusimamia vyema uchaguzi unaotarajiwa kugharimu Sh40.3 bilioni.

IEBC itahitaji pia Sh588 milioni kugharamia mahitaji ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Wawaniaji urais watakubaliwa kutumia kiwango kikubwa zaidi cha fedha, ambacho ni Sh4.4 bilioni.

Katika viti vilivyosalia, viwango ambavyo wanasiasa wanatakikana kutumia vitategemea ukubwa wa maeneo na idadi ya watu katika maeneo hayo.

Wawaniaji ugavana katika Kaunti ya Turkana ndio watakubaliwa kutumia kiasi kikubwa zaidi cha pesa miongoni mwa wagombeaji wote wa ugavana, ambacho ni Sh123 milioni.

Kaunti hiyo inafuatwa na Nairobi (Sh117.3 milioni), Marsabit (Sh114.8 milioni) na Wajir (Sh103.8 milioni).

Kaunti ambapo magavana watahitajika kutumia kiwango kidogo zaidi cha pesa ni Lamu (Sh21.9 milioni), na Tharaka-Nithi (Sh23.1 milioni).

Mwongozo huo wa kisheria unaonyesha kuwa, viwango ambavyo wabunge wataruhusiwa kutumia ni tofauti kuanzia Sh11 milioni katika baadhi ya maeneobunge kama vile Wundanyi, hadi Sh94 milioni eneobunge la Horr Kaskazini.

Katika wadi zote nchini, wale wanaotaka kuwania udiwani pia watakubaliwa kutumia viwango tofauti kuanzia takribani Sh2 milioni katika wadi nyingi hadi Sh17.9 milioni ilivyo katika Wadi ya Lokori/ Kochodin iliyoko Kaunti ya Turkana.

Kulingana na IEBC, viwango hivyo vyote ni tofauti na kiasi cha Sh17.7 bilioni ambacho vyama vya kisiasa vitakubaliwa kutumia kwa kampeni zao.

Pesa hizo hupangiwa kutumika kugharamia mahitaji kama vile malipo ya viwanja vya kampeni, vyombo vinavyotumiwa, matangazo, malipo ya maafisa na wahudumu wa kampeni na maajenti wa uchaguzi, uchukuzi, mawasiliano, usalama miongoni mwa mahitaji mengine.

Kwa kawaida, kampeni nchini kuanzia mashinani hadi urais huvutia mwembwe za kila aina.

Ni wakati huo ambapo wanasiasa hutaka kuonyesha ubabe wa jinsi wanavyoweza kusafiri kutoka pembe moja ya nchi hadi nyingine kwa saa chache wakitumia helikopta, na uwezo wao kutifua vumbi na tope kila wanapopitia barabara mbovu mashinani wakitumia magari makubwa makubwa.

Hata hivyo, kumekuwa na visa ambapo pesa hutumiwa kwa mambo yanayokiuka sheria za uchaguzi kama vile kugharamia uchochezi wa kisiasa, ghasia na kuhonga wananchi

“Visa vya uhongaji viliripotiwa hata katika chaguzi ndogo ambazo zilifanyika majuzi. Tunatarajia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atachukua hatua kuhusu madai yaliyotolewa. Taratibu za maadili ya uchaguzi zitatumiwa kikamilifu wakati wa kampeni. Wanasiasa watovu wataadhibiwa na vyama vya kisiasa vinavyovunja sheria vitaadhibiwa,” Bw Chebukati alisema Jumatatu.

Kulingana na IEBC, kulikuwa na visa 71 vya uvunjaji sheria ambavyo viliripotiwa mnamo 2017 ambapo watu 31 walishtakiwa na kupatikana na hatia.

Wakati huo huo, Bw Chebukati ameonya vyama vya kisiasa kwamba, orodha za wawaniaji ubunge na useneta watakazowasilisha lazima zizingatie sheria ya usawa wa jinsia, la sivyo hazitaidhinishwa.

Licha ya mjadala unaoendelea kuhusu uwezekano wa uchaguzi ujao kuahirishwa, mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba, Uchaguzi Mkuu utaandaliwa Agosti 9 kwa vile ndivyo inatakikana kikatiba.

You can share this post!

Nyota wa zamani wa Barcelona atua Vissel Kobe ya Japan

Machifu waeleza hofu kuhusu njaa