Habari Mseto

Ni upuuzi kusema makontena yanatumika kwa uuzaji wa mihadarati – Oguna

December 11th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

Muungano wa Vituo vya Uchukuzi wa Makontena nchini (CFSA) umepuzilia mbali matamshi ya msemaji wa serikali Cyrus Oguna kwamba vituo hivyo vinatumika kuleta mihadarati nchini.

Hii ni kufuatia matamshi ya Bw Oguna kwamba vituo hivyo vimekuwa pia vikikwepa kulipa ushuru.

Katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation, muungano huo unadai kuwa vituo hivyo hupokea mizigo katika hatua ya pili baada ya kutolewa kwenye bandari na hivyo matamshi hayo hayana msingi wowote.

“Madai haya yanashangaza sana kwani mizigo hiyo ukaguliwa kwanza katika bandari ya Mombasa ambayo pia ina maafisa wa KRA,mafias awa polisi na wale wa ujasusi,” walisema wanachama wa CFSA katika taarifa hiyo.

Waliongeza kuwa idadi kubwa ya maafisa wa CFS wamehudumu kwa zaidi ya miaka kumi na hakuna hata mmoja ambaye ashawahi kushtakiwa kwa madai hayo.

“Madai hayo yamekuwa kwa muda na inashangaza kwa nini vyombo vya sheria havijachukua hatua yoyote kufikia sasa.”

Waliitaka serikali kuangalia umuhimu wa vituo hivyo haswa kwa uchumi wa nchi na kuwapa nafasi kuendelea na kazi hiyo.

Waliongeza kuwa matamshi haya ni njama ya serikali katika kulazimisha huduma ya SGR kwa wanabiashara ambayo haina manufaa yoyote kwao ya kiuchumi.