TAHARIRI: Ni usaliti kulipia mabwawa hewa Sh80b

TAHARIRI: Ni usaliti kulipia mabwawa hewa Sh80b

Na MHARIRI

RIPOTI kutoka mahakamani zinaashiria kwamba Kenya huenda ikalazimika kulipa hadi Sh80 bilioni kwa sababu ya mabwawa ambayo hayakujengwa.

Kampuni ya CMC Di Ravenna Itinera Joint Venture imeelekea mahakamani ikitaka ilipwe mabilioni hayo na serikali kwa kukiuka mkataba walioweka wa kampuni hiyo kujenga mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Kampuni hiyo inasema ilikuwa tayari kujenga mabwawa hayo na kwamba ilikosewa vibaya kupokonywa nafasi hiyo wakati serikali ilipopiga breki ujenzi huo, sakata ya wizi wa pesa za mabwawa hayo ilipofichuka.

Itakumbukwa kuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Henry Rotich alifunguliwa mashtaka kuhusiana na kupotea kwa Sh65 bilioni za mradi huo wa mabwawa, kesi ambayo bado inaendelea kortini.

Ilivyo kwa sasa ni kwamba pesa ziliibwa na mabwawa hayakujengwa. Halafu sasa nchi inadaiwa kitita kingine cha Sh80 bilioni kwa kukiuka mkataba.

Ama kwa kweli, hii inatukumbusha ile sakata ya Anglo Leasing ambayo pia taifa lilipoteza zaidi ya Sh77 bilioni kwa namna hii wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Mwai Kibaki.

Pesa zililipwa watu fulani bila wao kutoa huduma kwa wizara zinazohusika na usalama.

Na ilipofika mwaka wa 2014, Rais Uhuru Kenyatta alisema Kenya imelazimika kulipa Sh1.6 bilioni kwa kampuni za Anglo Leasing zilizoshtaki serikali kwa kufutilia mbali kandarasi; akalipa faini hiyo ili Kenya iweze kupata mkopo wa Eurobond.

Inasikitisha kuona kwamba kila mwaka, kila miradi inaishia katika ubadhirifu wa pesa za umma. Katika taifa linalozongwa na umasikini wa kutisha, na mahangaiko makubwa yanayohusiana na njaa, maradhi na ukosefu wa elimu – matatizo ambayo yanastahili kutatuliwa na yeyote anayejiita kiongozi, inavunja moyo kuona badala yake ufujaji na kutojali kwa hali ya juu kukikithiri.

Tunatarajia kuona serikali ikionyesha kuhusu uchungu wa kulipa Sh80 bilioni fidia kwa kampuni hiyo ya CMC Di Ravenna inaypdai kukatiziwa kandarasi, kwa kufuatilia na kutwaa pesa zilizoibwa na kuhakikisha wezi wanaadhibiwa.

Kama inavyoshuhudiwa nchi zingine katika kukabili ufisadi, ushahidi huwa upo ila hauhitaji uzembe katika kuufuatilia na kuupanga katika hali inayokubalika kortini.

Hapo ndipo itaonyesha uwajibikaji kwa watu wa eneo la Arror na Kimwarer ambao wangali wanateseka kuwa Vila maji ya matumizi ya binadamu na mifugo, kutokana na kukwama kwa mradi wa mabwawa hayo.

You can share this post!

Usalama: Wakuu wahakikishia raia

Liverpool ni moto balaa EPL

T L