HabariSiasa

Ni usaliti mkubwa Raila kukutana na Uhuru – Miguna Miguna

March 11th, 2018 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAKILI mbishani Dkt Miguna Miguna Ijumaa alisema hatua ya Raila Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta na kutangaza ‘kumalizika kwa mgogoro wa kisiasa’ ni usaliti mkubwa kwa wafuasi wa upinzani.

Katika taarifa kutoka Toronto, Canada, Dkt Miguna alisema huo ulikuwa ni uamuzi wa Bw Odinga peke yake na ambao haukuwa na umuhimu wowote.

“Uamuzi wa upande mmoja Bw Odinga, usio na mantiki na usioelezeka ni kusaliti kampeni ya haki ya uchaguzi, kampeni dhidi ya utamaduni wa kutojali na ukiukaji wa haki za kibinadamu ambao umekuwa kawaida chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta na William Ruto sio wa haki,” alisema kiongozi huyo, aliyehamishiwa Canada na serikali wiki kadhaa zilizopita.

Dkt Miguna aliorodhesha visa vilivyotokea wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ambapo watu zaidi ya 300 waliangamia wakiwemo Baby Pendo, Stephanie Moraa (9), Geoffrey Mutinda (7), na aliyekuwa mkurugenzi wa habari, mawasiliano na teknolojia wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, marehemu Chris Musando, miongoni mwa wengine.

Alielezea dhuluma dhidi ya baadhi ya wanasiasa kuwa miongoni mwa sababu zinazomfanya kutounga mkono hatua ya Raila Odinga, na kuongeza kuwa waliokufa waliuawa kwa sababu walidhaniwa kumuunga mkono kiongozi huyo.

“Huku Raila Odinga na Uhuru Kenyatta wakisherehekea na kukumbatiana Nairobi, nimetengwa huku Canada kwa sababu nilimwapisha Bw Odinga Uhuru Park Januari 30, 2018,” alisema Dkt Miguna na kuongeza kuwa yumo humo sio kwa sababu ya kutaka lakini kwa kulazimishwa.

“Vinginevyo, makubaliano kati ya Uhuru Kenyatta na Raila ni usaliti kwa mamia ya wananchi wasio na hatia ambao wamepoteza maisha wakipigania demokrasia na kumtetea Raila Odinga baada ya kupokonywa ushindi 2007, 2013 na 2017,” alisema.

 

Udikteta

Alisema kuwa daraja walilosema kujenga litageuza Kenya kuwa taifa la kidikteta chini yake (Raila) na Rais Kenyatta.

Kwingineko, katika Kaunti ya Kitui nyumbani mwa Kinara mwenza wa NASA Kalonzo Musyoka, hatua ya Rais Kenyatta na Bw Odinga iliwakera wengi.

Kamwatu Malonza ambaye ni mhudumu wa teksi mjini Mwingi alisema kuungana kwa wawili hao ni usaliti mkubwa kwa vinara wenza kwani ni dhahiri kuwa kiongozi huyo wa upinzani alichukua hatua hiyo bila kuwahusisha.

“Hatukutarajia kuwa siku moja Raila angekubali kufanya kazi na serikali ya Jubilee, kwetu hatua aliyochukua ilikuwa usaliti mkubwa kwa kiongozi wetu Kalonzo Musyoka,”alisema Bw Malonza kwa ghadhabu.